26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SI AJALI TU, MAUAJI YA RAIA PIA YAKOMESHWE


JUZI, Rais Dk. John Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kumteua Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akichukua nafasi ya Dk. Mwigulu Nchemba.

Kabla ya uteuzi huo, Lugola alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Akizungumza wakati akiwaapisha manaibu waziri na makatibu wakuu wapya aliowateua katika mabadiliko hayo, Rais Magufuli pamoja na mambo mengine, aliweka msisitizo mkubwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, akionyesha kukerwa na ajali zinazotokea mara kwa mara na wahusika kutokuchukuliwa hatua madhubuti.

Katika msisitizo huo, Rais alisema amechoka kutoa rambirambi kutokana na ajali za barabarani kwa kutoa mfano kwamba ndani ya wiki mbili watu 40 wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) hajajiuzulu.

Tunampongeza Rais kwa kulipa uzito suala la ajali, ambalo limekuwa tatizo sugu lenye mwelekeo wa kushindikana licha ya kuwapo sheria na mbinu mbalimbali za kudhibiti mwendo kasi barabarani.

Pamoja na hayo yote, ajali bado zipo na zinaendelea kuua na kuteketeza watu na mali zao, huku wengine wakibakia walemavu wa kudumu na kuongeza mzigo kwa taifa.

Vilevile tunampongeza Waziri Lugola kwa kuaminiwa na Rais kubeba jukumu hilo zito linalohitaji weledi, nidhamu na busara ya hali ya juu, Watanzania waweze kupata huduma kwa haki kutoka kwenye vyombo vya dola anavyoviongoza.

Hata hivyo, ni siri iliyo wazi kwamba katika miaka ya karibuni taifa limeshuhudia maiti zikiokotwa na nyingine kuonekana zimefungwa kwenye viroba na kutupwa baharini au ziwani.

Matukio mengine ni ya watu kupotea bila kujulikana watekaji ni kina nani, wengine kupigwa risasi hadharani bila wahusika kukamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Matukio ya aina hiyo yamekuwa ni kero kubwa na kwa kiasi chake yamewakatisha watu tamaa na kufikia hatua ya kuona Jeshi la Polisi halifanyi kazi zake kwa weledi au limeshindwa kufanya kazi zake sawa sawa na inavyotarajiwa.

Matukio mengine ya ukiukwaji wa haki za binadamu ni pamoja na wingi wa mahabusu na wafungwa katika vituo vya polisi na magereza nchini.

Kwa sababu hiyo, tunashauri Jeshi la Polisi lijitathmini upya na lirudishe utaratibu wa awali wa kuwa rafiki wa raia ili kazi ya kubaini wahalifu iweze kutekelezeka kwa urahisi.

Tunachosema, kwa mfano, wakati mwingine vituo vya polisi vitumike kuunganisha jamii kwa kutoa elimu zaidi kuliko kutumia nguvu ambazo mara nyingi hazitoi matunda mema na hata kuonekana kama adui kwa wananchi.

Kutokana na umahiri wake, tunaamini waziri mpya, Lugola, ataziba upungufu ambao umeonekana kujitokeza na kuboresha penye udhaifu katika utendaji na utekelezaji wa majukumu.

Jeshi la Polisi lirejeshe hadhi yake ya kuwa rafiki wa wananchi na si kuogopwa na wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles