NA LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, ametoa siku 21 kwa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam kukamilisha ujenzi wa soko la muda la Kisutu kupisha ujenzi wa soko la kisasa katika eneo hilo.
Ujenzi wa soko hilo la ghorofa nne litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 1,500, utagharimu zaidi ya Sh bilioni 13.4 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.
Waziri Jafo alisema hayo juzi Dar es Salaam alipotembelea soko hilo kuangalia maendeleo ya ujenzi.
Soko ambalo wafanyabiashara wanatakiwa kuhamia lipo karibu na kituo cha mabasi ya mwendokasi cha Kisutu.
Waziri Jafo alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Msongela Palela, kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara sokoni hapo wakati wa ugawaji meza za biashara katika soko jipya kabla ya kuwakaribisha wapya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Pelela, alisema ujenzi wa soko jipya na la kisasa unatarajiwa kuanza hivi karibuni na tayari mkataba baina ya manispaa na mkandarasi umesainiwa tangu Juni 28, mwaka huu.
Alisema ujenzi wa soko hilo utajumuisha eneo la maegesho ya magari, benki na maeneo ya biashara mbalimbali zilizopo katika soko la sasa.
Kwamba gharama za awali za ujenzi wa soko hilo zilizotolewa mwaka 2014 zilikuwa Sh bilioni 12.1, lakini baada ya kufanyika kwa mapitio ya gharama za kihandisi mwaka huu, zimeongezeka hadi Sh bilioni 13.4.