Na Waandishi Wetu
MWANZO wa safari ya mwisho ya Daudi Ballali ulianzia pale aliporejea nchini kwa wito wa Rais wa Awamu wa Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alimfanya kuwa mshauri wake wa masuala ya uchumi katika Ikulu ya Magogoni.
Alirejea nchini akiwa na historia iliyotukuka kimataifa katika nyanja ya utumishi wa masuala ya uchumi baada ya kushika nyadhifa za juu kwenye Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Uchunguzi wa MTANZANIA kuhusu historia ya awali ya Ballali umeonyesha kuwa alisomeshwa kwa shida na marehemu baba yake, mzee Timoth Said Balali, aliyekuwa mtumishi wa ndani wa wazungu ambaye baadaye alikuja kuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Kidugala, kabla hajawa dereva wa Shirika la Reli Tanzania kwa miaka mingi.
Taarifa zilizokusanywa kutoka katika Kijiji cha Luganga, mahali alikozaliwa na kukulia marehemu Ballali, ambaye nyumba yao inaangaliana na kambi ya jeshi, zinaeleza kuwa marehemu mama yake alifariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kisukari kwa muda mrefu.
Mama yake alikuwa akiitwa Rachel Benamanga, mwenyeji wa Mkoa wa Morogoro, aliyetoka katika kabila la Wambunga na ndiye aliyekuwa mke mkubwa wa marehemu mzee Timoth Ballali, ambaye kwa asili naye alitokea mkoani Morogoro na alihamia Iringa akiwa mtumishi wa ndani wa wazungu akiambatana na wakeze wawili waliomzalia watoto 20.
Ndugu wa marehemu mzee Timoth waliozungumza na MTANZANIA kuhusu historia ya familia yake walisema kuwa mke wake mdogo ambaye pia ni marehemu, alijulikana kwa jina la Christina na alijaliwa kuzaa watoto 10, huku marehemu Rachel naye akijaliwa kuwa na idadi kama hiyo ya watoto, akiwemo marehemu Ballali.
Kwa mujibu wa maelezo yao hayo, marehemu Timoth Ballali, alizaliwa mwaka 1922 na yeye alizaa watoto 20 na alimzaa marehemu Ballali mwaka 1942, wakati huo akiwa kijana wa miaka 20 tu.
Wakimuelezea marehemu Ballali, walisema alipofikisha umri wa kwenda shule, alipelekwa Shule ya Misheni ya Tosamaganga na alipohitimu elimu ya msingi alichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule hiyo hiyo.
Wazee wachache wa Kijiji cha Luganga waliozungumza na MTANZANIA, walimuelezea marehemu Ballali kuwa alikuwa mwanafunzi aliyependwa sana na walimu wake kwa sababu ya uwezo wake wa kumudu masomo darasani.
Ingawa hakuna hata mmoja kati ya waliohojiwa aliyedai kusoma na marehemu Ballali darasa moja, kauli zao kuhusu mwenendo wa Ballali darasani zilifanana, kwa maelezo kuwa alisoma shule ya msingi na sekondari kwa muda wa miaka kumi tu, kwa vile alikuwa akirushwa madarasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa akili.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye nyaraka za kumbukumbu za watumishi wa umma umeonyesha kuwa akiwa na miaka 18, marehemu Ballali alijiunga na Chuo Kikuu cha Howard kilichoko nchini Marekani, ambako alisoma na kuhitimu shahada yake ya kwanza katika masuala ya uchumi.
Kumbukumbu hizo zinaonyesha kuwa baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza, baadaye mwaka 1964 alijiunga na Chuo Kikuu cha Kikatoliki kilichopo Washington, Marekani ambako alihitimu shahada ya uzamili kabla hajachukua shahada ya uzamivu mwaka 1967.
Mwaka huo huo baada ya kuhitimu masomo yake alirejea nchini na kujiunga na BoT akiwa mchumi na alifanya kazi katika taasisi hiyo hadi 1976 alipojiunga na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Wasifu wa Ballali ambao gazeti hili limeuona, unaonyesha kuwa kati ya 1979 na 1982 alifanya kazi katika ofisi za IMF nchini Ghana akiwa mchumi na baadaye alipandishwa cheo kuwa mchumi mwandamizi kwenye ofisi hizo hizo mwaka 1982 na kudumu na nafasi hiyo hadi 1984.
Alihamishiwa nchini Zimbabwe mwaka 1984, akiwa na wadhifa wake huo huo na 1986 aliteuliwa kuwa Msaidizi Mkuu wa Divisheni, akiongoza Kitengo cha Mashauriano na Uongozi wa Marekebisho ya Programu katika ofisi za IMF, mjini Washington, Marekani.
Ni kipindi hicho ndipo alipokabidhiwa jukumu la Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kusimamia Mageuzi ya Kiuchumi katika nchi za Asia, Afrika na Caribbean.
Aliitwa kurejea nyumbani mwaka 1997 na Mkapa, ambaye alimfanya kuwa mshauri wake wa masuala ya uchumi, kabla ya kumteua kuwa Gavana wa BoT mwaka 1998.
Wakazi wa Kijiji cha Luganga wanaeleza kuwa baada ya kurejea nchini na kuteuliwa kuwa Gavana, marehamu Ballali alikuwa akimtembelea kila mara marehemu baba yake na kwamba hata alipofariki aliongoza mazishi yake katika makaburi ya familia.
Waandishi wa gazeti hili waliofika Kijiji cha Luganga kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa utata uliogubika kifo cha marehemu Ballali, walifanikiwa kuliona kaburi la marehemu mzee Timoth Ballali aliyefariki dunia mwaka 2000 na habari zaidi kutoka ndani ya familia zilielezwa kuwa watoto wake walio hai ni 14 na sita walikwishafariki, akiwemo Ballali.
Watatu kati yao wanatajwa kuwa ni wakazi wa mkoani Iringa, mmoja anaishi Kigoma na waliosalia wana makazi yao jijini Dar es Salaam.
Kashfa ya EPA
Marehemu Ballali aliteuliwa na rais wa wakati huo, Mkapa, kuwa Gavana wa BoT baada ya kufanya naye kazi kama mshauri wake wa masuala ya uchumi katika Ikulu ya Magogoni. Hiyo ilikuwa mwaka 1998.
Akiwa katika wadhifa huo, ndipo taarifa za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa BoT, zilipoanza kutolewa kwenye mitandao na watu wasiojulikana.
Ingawa hadi sasa hakuna taarifa sahihi za mtu au kikundi cha watu kilichoibua kashfa hiyo kwa mara ya kwanza katika mitandao ya kijamii, zipo tetesi kuwa kundi dogo la wanausalama ndilo lililohusika katika jambo hilo.
Taarifa za awali wizi huo ziliwataja kuhusika baadhi ya wafanyabishara wakubwa, wanasiasa wenye majina makubwa na jina la Ballali liliguswa kwenye kashfa hiyo kama mtu muhimu anayejua jinsi mipango ya wizi huo ilivyofanyika kulingana na wadhifa wake wa ugavana aliokuwa nao BoT.
Hata hivyo, wapo waliolijumuisha moja kwa moja jina la Ballali katika kashfa hiyo kubwa na ya kwanza ya aina yake iliyopata kulitikisa taifa, hususan wanasiasa wa kambi ya upinzani waliokuwa wakidai kuwa alilazimishwa kushiriki katika mipango hiyo ya wizi kutokana na shinikizo la wakubwa waliokuwa wakisaka fedha zitakazowasaidia kuendesha kampeni za uchaguzi.
Fedha iliyotajwa kuibiwa katika akaunti ya EPA ni Sh bilioni 135 na haraka haraka, kundi la wanasiasa machachari wa kambi ya upinzani likiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Karatu wakati huo, Dk. Willbrod Slaa, liliibeba kashfa hiyo na kwenda kuibwaga bungeni ambako iliibua mzozo mkubwa.
Kwa upande mwingine, baadhi ya vyombo vya habari navyo vilizama katika kuchunguza ukweli wa tuhuma hizo na kuziripoti, huku Bunge na Serikali vikajitihadi bila mafanikio kuzima upepo wa kashfa hiyo.
Ni sekeseke hilo ambalo lilimlazimisha Ballali kuitisha mkutano na waandishi wa habari hapo BoT, ili kulitolea ufafanuzi, huku akitumia pia mwanya huo kulisafisha jina lake ambalo lilikuwa likitajwa kuhusika.
Hata hivyo, hatua yake ya kuzungumza na wanahabari haikusaidia kupunguza joto la kashfa hiyo, hali iliyomlazimu kwenda bungeni Dodoma kwa wito maalumu na baadaye kujibu kile ambacho kilikuja kuitwa na wadadisi wa mambo kuwa ni mashtaka ya Ballali katika sakata la wizi wa mabilioni ya EPA.
Usikose kusoma mashtaka hayo kesho na mazingira yanayoonyesha kuwako kwa wingu jeusi katika kifo chake.