Mwandishi Wetu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo, wamekubaliana kuweka mgombea mmoja wa ubunge katika Jimbo la Buyungu.
Licha ya hayo, vyanzo kutoka Chadema vinadai ACT-Wazalendo imejiunga rasmi na Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) ambayo Chadema ni sehemu ya muungano huo na moja ya makubaliano ya muungano huo mpya uliopewa jina la ‘Ukawa Ndogo’ ni kuweka mgombea kuanzia jimbo hilo la Buyungu hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Hatua hiyo imefikiwa leo Mei 30, mjini Kigoma baada ya vikao kadhaa kati ya vyama hivyo viwili wakati wa ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Kasuku Bilago aliyefariki dunia jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo, akitoa salam za rambirambi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema vyama hivyo vimekubaliana hawatapingana wataweka mgombea mmoja.
“Hata kama vyama vingine vitakengeuka lakini Chadema haitaingia kwenye mgogoro huo na tutafanya hivyo hadi katika Uchaguzi Mkuu,” amesema Mbowe.
Hata hivyo, hatua ya kujiunga na Ukawa imepingwa na Zitto akidai chama chake hakijajiunga na Ukawa isipokuwa wamekubaliana kuweka mgombea mmoja na kushirikiana hadi mwisho.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mtanzania Digital, Zitto amesema kwa heshima ya Bilago na undugu waliokuwa nao nafasi hiyo ameiachia kwa Chadema.
“Sijui mmetoa wapi hiyo ya Ukawa, kwanini kila umoja wa wapinzani ninyi mnaita Ukawa?
Kujiunga Ukawa ni mchakato. Chama ni taasisi, lazima vikao vya chama vikae chama chetu si sehemu ya ukawa.
“Chama chetu kinataka muungano mpana zaidi ya vyama vya Siasa. Tuliamua kuwa mwaka 2018 utakuwa mwaka wa kujenga mashirikiano,” amesema.
Aidha, amesema wamekubaliana kuweka mgombea mmoja anayekubalika na wananchi wa Buyungu na kufanya kampeni kwa pamoja hadi ushindi.