25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

LUGHA NZURI NI SILAHA YA KUKUJENGEA UAMINIFU

Na Christian Bwaya


UNAYE rafiki wa siku nyingi lakini miaka kadhaa imepita hamjawasiliana, leo asubuhi amekuandikia ujumbe mfupi wa maneno akisema: “Habari za siku ndugu yangu, unaendeleaje na maisha? Hatujawasiliana muda mrefu, nimekukumbuka sana rafiki yangu.

“Ulikuwa mtu wa maana enzi za shule, sitakusahau hata siku moja. Nilipata taarifa za uteuzi wako, Hongera , kwa jinsi ninavyokuamini nilijua utafika mbali.

“Lilikuwa suala la muda kabla hujapata nafasi uliyo nayo, ninajisikia fahari kuwa rafiki yako na ninakutakia mafanikio makubwa kwenye majukumu yako mapya.”

Ungejisikiaje kusikia maneno hayo? Bila shaka ungejisikia vizuri, Sio siri binadamu tuna hitaji kubwa la kutambuliwa, unapoona kuna mtu anakuelewa moyo wako unachangamka lakini fikiria rafiki yako huyo anaendelea kama ifuatavyo:

“Ninatarajia kuoa Julai, harusi itafanyikia nyumbani kwa wazazi wangu Tukuyu. Ningeshukuru kama ungenichangia ndugu yangu, tumetoka mbali. Kiwango cha mchango ni Sh 50,000 kwa mtu mmoja. Kama una mwenza wako ni Sh 80,000 shukrani.”

Ungejisikiaje kusoma sehemu hiyo ya pili ya ujumbe wake? Labda ungefurahi, sifa na pongezi alizotanguliza inawezekana zikawa zimekugusa kiasi cha kukufanya ujisikie kuwajibika kukubali ujumbe unaofuata. Lakini kwa wengine, sehemu hiyo ya pili inaweza kuwafanya wakajisikia vibaya. Kwao, ombi hili limekuja kwa namna inayojenga taswira mbaya.

Mwombaji huyu mathalani, anaweza kuonekana si mtu mkweli. Ametanguliza sifa na pongezi mwanzoni kama namna ya kukuvuta usikilize ombi lake, kwa maana hiyo hakumaanisha kukupongeza kwa dhati bali kukulaghai tu uvutike kumsaidia. Hisia kama hizi zinaweza kufanya si tu sifa na pongezi zake zionekane ni utapeli wa mchana kweupe, bali pia lionekane halina maana yoyote.

Hebu fikiria mtu huyu aanze tofauti kidogo kama ifuatavyo: “Habari za siku ndugu yangu, unaendeleaje na maisha? Hatujawasiliana muda mrefu, unajua ninafanya maandalizi ya kufunga ndoa Julai.

“Mambo hayajakaa vizuri, imebidi nikumbuke watu wanaoweza kunisaidia, nitashukuru kama utanichangia chochote ulichonacho kuwezesha shughuli hii muhimu.”

Hapa umeelewa moja kwa moja kwamba lengo la yeye kukutafuta ni kuomba msaada, hata akiendelea na pongezi hutapata shida kumwelewa.

Tunachokiona hapo ni nguvu ya mawasiliano, Usipojua namna ya kupangilia hoja zako vizuri, unaweza kumfanya msikilizaji akakuelewa vingine.

Fikiria mfano huu mwingine umegundua mtu unayefanya naye kazi muhimu amekosea na unataka aelewe kosa lake abadilike. Unamwambia: “Nakukubali kwa kazi zako, unao uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yako. Sina wasiwasi na wewe kabisa. Ila nimeona kazi uliyonitumia leo, naona kuna upungufu kidogo, naomba urekebishe tuwatumie wale jamaa mchana wa leo.”

Hapa tunaona lengo lako halikuwa kumsifia bali kumweleza upungufu uliouona kwenye kazi yake. Sifa ulizotoa ilikuwa ni namna tu ya kumwandaa kusikia upungufu alionao. Ingawa mbinu hii inaweza kufanya kazi kwenye baadhi ya mazingira kama yale ambayo anayesikia anapata mrejesho wa tathmini ya kazi yake kwa ujumla, lakini inapotumika bila uangalifu inaweza kueleweka kama ‘kucheza na akili za mtu’ na hivyo kupunguza uwezekano wa kupokelewa vizuri.

Kinyume chake ni kumpa mhusika ujumbe halisi vile ulivyo bila kuzunguka mbuyu. Ingawa ni kweli anaweza kujisikia vibaya mwanzoni, lakini ukifanya hivyo hatakuwa na wasiwasi na maneno yako na atakuamini zaidi. Muhimu ni kutumia lugha yenye staha inayojali heshima yake badala ya kumpamba kwa sifa unazojua kabisa huzimaanishi.

Mfano unaweza kumwambia, “Nimesoma kazi uliyonitumia leo, sijaridhika nayo. Nafikiri tunaweza kuifanyia kazi zaidi ili wale jamaa wasitusumbue. Kuna moja, mbili, tatu naomba ufanyie kazi. Nakuamini, najua utafanyia kazi maeneo hayo.” Uwezekano wa ujumbe huu kuaminika na kufanyiwa kazi ni mkubwa zaidi kuliko sifa zinazomwandaa mtu kusikia kasoro.

 

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles