Johanes Respichius, Dar es Salaam
Wadau wa kilimo nchini wameitaka Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kutambua nafasi ya mwanamke na kumpa kipaumbele kwa kumwekea mazingira wezeshi ili kufanya kilimo chenye tija.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa semina ya Jinsia na Maendeleo (GDSS) ulioandaliwa na Mtandao Kijinsia Tanzania (TGNP) kwa ajili ya kujadili nafasi ya mwanamke katika bajeti ya Wizara ya Kilimo 2018/19.
Akizungumza katika semina hiyo, Ofisa Programu Msaidizi Idara ya Utafiti, Elimu na Uchambuzi, Jackson Malangalila, amesema umefika wakati wa serikali kumfanya mwanamke kuwa kipaumbele muhimu katika maendeleo ya kilimo hasa katika zama hizi za uchumi wa viwanda.
“Zaidi ya asilimia 75 ya wanawake nchini ni wakulima tena wakulima wadogo lakini wamekuwa na changamoto kubwa ya kukosa pembejeo muhimu kuendesha shuguli hiyo jambo ambalo limekuwa likiwakosesha faida na kuendelea katika hali ya umasikini,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sauti jamii Kipunguni, Selemani Bishagazi, amesema kitendo cha bajeti ya Wizara ya Kilimo kupunguzwa kutoka Sh bilioni 150.253 mwaka 2017/18 hadi Sh bilioni 98.119 ni kuelekea kushindwa kwa serikali kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Kwa bajeti hii ambayo imepitishwa hivi karibuni bungeni mjini Dodoma ndio kuelekea kushindwa kwa serikali kufikia uchumi wa viwanda maana baada ya kuendelea kuipa kipaumbele wameishusha kwa asilimia 34.69 jambo linaloondoa matumaini,” amesema Bishagazi.