30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CCM ATAKA MFUMO MPYA KUNUSURU PAMBA

Mwandishi Wetu, Dodoma

Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga (CCM), ameitaka serikali kutengeneza mfumo mpya wa kuhakikisha zao la pamba linafanya vizuri sokoni.

Aidha, amelalamikia uendeshaji wa vyama vya ushirika ambapo amesema ushirika uliopo sasa uko hoi kwani hata maghala yao yalishauzwa.

Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2018/19, Silanga amesema bei ikiwa nzuri na kukiwa na pembejeo za kutosha watazalisha kilo milioni 2.4 kwa mwaka.

“Kwa sababu mikoa inayolima pamba ni 17 na tunazo wilaya 56, utaona tu kwamba hata uzalishaji kwa mwaka huu umepiga hatua ukigawanya wastani wake ni kama kila wilaya imezalisha tani 10, ambapo tukisimamia jukumu hili tukalibeba wote tutafanikiwa,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, Silanga amesema hivi karibuni, Waziri Mkuu alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuunda vikundi lakini kilichofuatia ni Mrajisi kutengeneza ushirika wake wa miaka 20 ambao wakulima wanauchukia kiasi kwamba hata sasa hivi ukisema ushirika wanakimbia.

“Mheshimiwa Waziri, katika bajeti yako umesema umeamua kutoa mfuko wa wakfu katika zao la pamba lakini kwenye kikotoo huku umeandika Sh 100, sasa ungetupa majibu tunafanya kitu gani.

“Tukiweka uzalishaji mzuri na usimamizi mzuri, wakulima wetu wa pamba hawasukumwi kwa sababu ni wajibu wao na ni biashara yao lakini kadri tunavyotaka kwenda tunaweza tukatengeneza mazingira ya kuua zao la pamba na itafia hapa Dodoma.

“Tunarajia kuvuna kilo milioni moja mwaka 2020 na kuendelea, lakini kwa mwendo huu wakulima watakataa kulima na wataacha kulima.

“Nakuomba waziri tafuta mfumo mzuri na hasa zaidi hili jambo, sisi kule kwetu tulikuwa na Chama Kikuu cha Ushirika kinaitwa Shirecu, lakini baada ya Ofisi ya Mrajisi kuingia pale alitengeneza madudu hadi na maghala yetu yakauzwa ambayo yalikuwa makubwa pale Dar es Salaam.

“Lakini leo mrajisi huyu amerudi tena na mfumo ule ule ambao umewatesa wakulima wetu na imewakatisha tamaa. Ningeomba jambo hili tulichulue kwa umakini mkubwa wenye tija na tujaribu kuweka mifumo ambayo itakuwa rafiki kwa wakulima ambao wanazalisha kwa moyo mmoja na wanapata fedha zaidi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles