Gabriel Mushi, Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba kulieleza Bunge sababu za wabunge wa viti maalumu kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo wanayowakilisha.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2018/19, leo Mei 4, bungeni jijini Dodoma Upendo amesema polisi wamekuwa wakikandamiza demokrasia ikiwamo kuwazuia kufanya mikutano kwenye mikoa yao.
“Kaka yangu, Mwigulu kama ulitegemea kuwa rais siku moja, wabunge wa viti maalumu wapo humu kwa mujibu wa Katiba, inazungumza uwepo wa wabunge wa viti maalumu ambao majina yao yanapendekezwa na vyama vyao,” amesema Peneza anayetoka mkoa wa Geita na kuongeza, lakini mimi pamoja na wabunge wengine, tumekuwa tukizuiwa kufanya mikutano ya hadhara, wabunge tunaambiwa tufanye kazi vyumbani? Wabunge wa viti maalumu tunadhalilishwa, mtuache tufanye kazi na mwisho wa siku tunalipwa fedha.”
Amesema kupitia mikutano ya hadhara ndiko ambako wanaibuka wanawake na vijana akiwamo yeye alivyoibuka na kutokufanya na kuonekana tutawezaje kuonekana na hapo ndipo tutaruhusu ngono na nini na mnaathiri ndoto za wanawake na vijana.
“Katika majibu yako baadaye leo ya Waziri Mwigulu, usinijibu kama ulivyofanya wakati bajeti ya Katiba na Sheria, kama unataka kuwa Rais siku moja, onyesha njia,” amesema.