Hadija Omary, Lindi
Baadhi ya madiwani katika Manispaa ya Lindi, wamesusa kuchangia hoja kwenye kikao robo tatu ya mwaka cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo kwa siku mbili mfululizo, kwa madai kuwa Mwenyekiti anaendesha vikao kidikteta.
Madiwani hao ambao wamekuwa wakiingia katika vikao hivyo kama kawaida lakini wakati wa kuchangia hoja au kuuliza maswali wamekuwa wakikaa kimya.
Naibu Meya wa halmashauri hiyo, Asna Kawanga baada ya kubaini wajumbe wa kikao hicho kuwa na muonekano usio wa kawaida aliliomba baraza na mwenyekiti wa kikao hicho kuangalia sababu iliyowafanya baadhi ya wajumbe kutochangia kwa muda wa siku mbili za kikao hicho.
“Kitendo cha wajumbe kususia kuchangia kikao hicho inaonyesha kuna tatizo, hivyo ni vyema uongozi na baraza kwa ujumla likatafuta njia ya kutatua hali kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Lindi,” amesema.
Meya wa Manispaa hiyo, Mohamedi Lihumbo amesema kikao cha baraza kinaendeshwa kwa sheria, kanuni na taratibu, hivyo kama wajumbe wana jambo taratibu za kufuata zipo.
Akizungumzia hali hiyo, Diwani wa Kata ya Ndoro, Issa Luwono (GIF), amesema wameamua kukaa kimya baada ya kuona kuna taratibu zinakiukwa ikiwamo kuwanyima haki ya kuchangia na uhuru wa kuuliza maswali baadhi ya wajumbe kutoka kambi ya upinzani.
Amesema miongoni mwa hoja na maswali hayo yangeweza kutoa mwanga wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kata zao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Wailesi, Alifa Mbaruku (CCM), ambae aliamua kuliondoa swali lake ndani ya kikao cha baraza hilo amesema amefanya uamuzi huo kwa kuwa mara kwa mara alijaribu kuliuliza na kutaka kufahamu juu ya utekelezaji wake lakini utekelezaji hakuna.