BERLIN, UJERUMANI
RIPOTI iliyotolewa na Shirika la Waandishi wasio na Mipaka (RSF) imemtuhumu Rais wa Marekani, Donald Trump na mataifa ya Urusi na China kuwa tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari duniani.
Aidha ripoti hiyo ya mwaka 2018 imesema kushamiri kwa siasa za kizalendo barani Ulaya kumechangia kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari eneo hilo, ambalo awali lilikuwa salama zaidi.
Kwa mujibu wa ripoti, uhasama dhidi ya waandishi na vyombo vya habari ni kitisho kikubwa kwa demokrasia duniani kote ikiwamo Ulaya.
Kati ya nchi tano za juu ambako hali ya uhuru wa vyombo vya habari imeshuka zaidi, nne kati ya hizo ziko Ulaya, ambazo ni Malta, Slovakia, Jamhuri ya Czech na Serbia.
Shirika hilo limeonyesha wasiwasi hasa kuhusu mauaji ya mwandishi Daphne Caruana Galizia wa Malta, yaliyofuatiwa na mauaji ya mwandishi mwingine wa habari za uchunguzi, Jan Kuciak miezi mitano baadae.
Kutokana na kushamiri kwa siasa za kizalendo na viongozi ‘wababe’ Ulaya itaendelea kushuka viwango, limeonya shirika hilo.
RSF imesema chuki dhidi ya wanahabari ‘si tu katika utawala wa Uturuki na Misri bali pia imeingia katika maeneo mengine.
Pia ripoti hiyo imeonesha wasiwasi juu ya “udhibiti na ufuatiliaji” wa wanahabari nchini China huku Rais Xi Jinping akizidisha udhibiti wa vyombo vya habari katika maeneo ya bara la Asia.
Ripoti hiyo inasema Raism huyo wa China anakaribia kuwa toleo la kisasa la utawala wa kiimla.
Norway imeendelea kushikilia nafasi ya juu katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka wa pili mfululizo huku Korea Kaskazini ikisalia katika nafasi ya mwisho kati ya nchi 180 zilizopimwa viwango hivyo.
Nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika orodha hiyo ni Gambia, ilipanda kwa nafasi 22 hadi kufikia nafasi ya 122.