Gabriel Mushi, Dodoma |
Licha ya Watanzania kulalamikia tozo za ada kubwa kwa shule binafsi, Serikali imesema bado inaendelea na majadiliano wamiliki wa shule hizo kuhusu uratibu wa ada elekezi pamoja na viwango vya ufaulu.
Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma leo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Olenasha wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Paschal Haonga (Chadema) aliyetaka kujua kuondoa kodi zisizo na tija kwa shule binafsi.
Pia Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) alitaka kujua kwanini serikali isiwaachie wamiliki shule binafsi wajipangie viwango vya ada na ufaulu.
Akijibu maswali hayo Olenasha alisema kwa sasa serikali inaendelea na majadiliano na wamiliki wa shule binafsi kuhusu ada elekezi badala ya kuwapangia kwani shule binafsi ni biashara ambayo ina gharama katika uendeshaji.
Aidha, amesema serikali itaendelea kuzibana shule binafsi katika mambo mbalimbali ikiwamo viwango vya ufaulu kwa kuwa ni suala la kisera lakini serikali itaendelea kushirikiana na wamiliki wa shule binafsi katika mambo mbalimbali ili kutovunja sheria.