KAMILI MMBANDO-DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) ameeleza kuwa tatizo la mafuriko Dar es Salaam ni wanasiasa kutothamini kazi za wataalamu wa mipango miji.
Profesa Tibaijuka ameyaeleza hayo wakati huu ambao jiji la Dar es Salaam limekumbwa na adha kubwa ya mafuriko kutokana na mvua inayoendelea kunyesha na kusababisha vifo kadhaa, watu wengine kukosa mahali pa kuishi na barabra kufungwa hasa barabara ya Morogoro eneo la Jangwani.
Katika taarifa yake aliyoituma kwenye mitandao ya jamii juzi, Mbunge huyo alisema tatizo la mafuriko halitokani na wataalamu bali ni wanasiasa kukosa utamaduni wa kuheshimu wataalamu na wananchi kutaka njia rahisi.
Alisema tatizo hilo la mafuriko halitaweza kuisha kwa sasa mpaka utakapotekelezwa mpango maalum wa jiji hilo (master plan) wa mwaka 1979 wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere ambao ulionyesha jinsi ya kumaliza tatizo la mafuriko Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ya Profesa Tibaijuka ilieleza kuwa kama hakutakuwapo na nidhamu ya kuheshimu wataalamu wa mipango miji, mafuriko yataendelea kuwa tatizo sugu na la muda mrefu katika jiji hilo.
“Tatizo si mvua kubwa, tatizo ni kuziba njia za asili zinazotiririsha maji kwenda baharini.
“Nilipokuwa Wizara ya Ardhi, nilijitahidi kuokoa Bonde la Mto Msimbazi kwa mujibu wa master plan1979 ambayo ilikuwa ni ya Nyerere, sikuweza kufanikiwa… bonde likaendelea kujengwa na maji hayana njia nyingine ya kufika baharini.
“Fikiria Bonde la Msimbazi (mto) ndiyo njia pekee ya maji yote yanayotoka Pugu, Hills, Ukonga, Airport, Tazara, Tabata, Kigogo, Magomeni, Ilala kufika Jangwani katika mizunguko hadi daraja la Salendar.
“Vile vile maji kutoka Ubungo, Manzese, Tandale, Magomeni Kagera, Kinondoni Hananasifu, Muhimbili hadi Jangwani na njia ni hiyo tu moja huku kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kukiwa na Mto Mbezi, Mto Mlalakuwa na Mto Mdumbwi na eneo la Kawe likiwa limejengwa kwenye njia za maji,” alieleza.