NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Dylan Kerr, ameridhishwa na viwango vya kiungo, Justice Majabvi raia wa Zimbabwe na kipa Muivory Coast, Vincent Angban, wanaosaka nafasi ya kusajiliwa na timu hiyo.
Mwingereza huyo amesema hayo baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya SC Villa ya Uganda kwenye sherehe za Simba Day na kushinda bao 1-0 juzi, lakini amewapa mtihani nyota hao akiwataka waonyeshe makubwa zaidi.
“Nimefurahishwa na baadhi ya vitu kwenye utendaji wao wa kazi uwanjani, lakini sijafurahishwa na baadhi ya vitu vyao, huu ni mpira, mimi kila siku nataka ubora zaidi, nitazidi kuwaangalia,” alisema.
Wawili hao walianza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kabla ya Majabvi kutolewa kipindi cha pili na kuingia Awadh Juma mfungaji wa bao pekee la Simba.
Kerr alizidi kuliambia MTANZANIA kuwa bado hajaridhishwa kwa asilimia 100 namna kikosi chake kinavyocheza, akidai kuwa anahitaji kiwango bora zaidi.
“Unaona kama leo (juzi) kipindi cha kwanza wachezaji wangu hawakucheza vema, lakini kipindi cha pili tukarejea mchezoni. Wachezaji wangu wameshindwa kabisa kutumia nafasi walizopata.
“Naamini atakaporejea Mkude (Jonas) ambaye ni majeruhi timu itaimarika zaidi, kwani amekuwa akipambana vema uwanjani na kuichezesha vema timu,” alisema.
Akizungumzia kiwango cha kiungo Mwinyi Kazimoto, aliyeingia kipindi cha pili, Kerr alisema: “Mwinyi bado hayuko fiti na nimeshamweleza hilo, kikubwa alipoingia nilimpa maelekezo ya kucheza kwa kuchukua mpira na kuichezesha timu, bila kuhangaika sana, amefanya vizuri naamini ataimarika zaidi.”
Beki huyo wa zamani wa Leeds United, alisema kesho anatarajia kukaa na uongozi wa timu hiyo ili kujadili programu nzima ijayo na kuona kama watapata mechi nyingine za kirafiki kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Septemba 12, mwaka huu.
Wakati huo huo, Simba ipo kwenye mchakato wa kuwafanyia majaribio washambuliaji Makan Dembele kutoka Mali aliyewahi kuzichezea JS Kabylie pia Raja Casablanca ya Algeria na Mrundi Kevin Ndayisenga, ambaye ni mfungaji namba mbili Burundi.
Baada ya kuumia kwa kipa Ivo Mapunda, Simba imekuwa ikimjaribu Angban ili kuliongeza nguvu eneo hilo lakini tayari pia imemshusha kipa Ricardo Andrade kutoka Ureno, aliyewahi kuichezea timu ya Sporting CP ya huko.
Simba inahaha kurudisha heshima yake msimu ujao wa ligi ambayo imepotea kwa miaka mitatu sasa ikishindwa kutwaa taji wala kushiriki michuano ya kimataifa.