32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

PROF LIPUMBA APUUZWE-MAALIM SEIF


Na CHRISTINA GAULUHANGA- DAR ES SALAAM  |  

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wanachama wa chama hicho kumpuuza Mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake kwa madai wanatumika kisiasa.

Kauli hiyo, imekuja siku chache baada ya Lipumba kutangaza maazimio ya Kamati Tendaji na mikakati ya chama hicho kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema propaganda za Lipumba na kundi lake ni dhaifu, hivyo wananchi wanatakiwa kuzitupilia mbali.

Alisema hadi sasa hawatambui uchaguzi wowote uliofanyika au uliotangazwa unaohusu chama hicho zaidi ya ule wa mwaka 2014 na wanasubiri ridhaa ya Baraza Kuu la chama hicho kwa uchaguzi mwingine.

“Chama chetu kipo imara, tumejipanga na tutatangaza tarehe ya uchaguzi baada ya agizo kutoka Baraza Kuu kwa Kamati Tendaji ya Taifa, kwa sasa tunaoutambua ni ule wa 2014 tu,” alisema Maalim Seif.

Alisema hadi sasa Baraza Kuu halijaanza jambo lolote linalohusu maandalizi ya uchaguzi, hivyo viongozi wa CUF ngazi zote wanatakiwa kupuuza kauli za Lipumba.

Maalim Seif alisema anamfahamu Lipumba muda mrefu na mambo anayoyafanya hivi sasa yanaonyesha dhahiri anatumika na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Sisi wengine tunamfahamu Lipumba kwa muda mrefu, lakini mambo anayoyafanya hivi sasa yanadhihirisha wazi anafanya kazi za CCM,” alisema Maalim Seif.

Alisema Lipumba amepoteza mwelekeo na ndiyo maana hata alivyokwenda Visiwani Zanzibar hivi karibuni, hakuna hata waliompokea kwa shangwe tofauti na miaka ya nyuma.

Maalim Seif alisema vurugu anazozifanya na wafuasi wake zina lengo la kukiua chama, lakini wao wapo imara huku akiwataka wanachama wake kuwa wastahamilivu.

Alisema anafahamu nguvu kubwa anayoipata Lipumba katika ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa ambako hivi sasa wamejenga mahusiano kama mapacha.

“Tunafahamu ofisi ya Msajili inavyombeba Lipumba, kwani ruzuku ya CUF ni Sh bilioni 2.5, lakini hadi sasa Lipumba tayari amepewa zaidi ya Sh bilioni 3 na ofisi hiyo,” alisema Maalim Seif.

Aliongeza ni muda mwafaka kwa wanachama kuwafichua wahujumu wa chama hicho na wasikubali kuchokozeka, huku wakijitahidi kuwadhibiti wenye nia ya kukivuruga chama hicho.

Pia alisema katika kikao cha Kamati Tendaji, imedhamiria kufuatilia kwa makini ukiukwaji wa haki za kibinadamu.

Alisema pia wataendelea kuikumbusha Serikali na vyombo vya usalama jukumu lao la msingi la kulinda raia na mali zao.

Aliwapongeza mawakili wanaosimamia kesi zao ambazo zinaendelea zikiwa chini ya msimamizi Kaimu Katibu Mkuu Bara, Joram Bashange ambaye amejitolea kwa dhati.

Machi 22, mwaka huu, Lipumba alitoa maazimio ya Kamati Tendaji ya CUF, ya kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020.

Pamoja na mambo mengine, alisema kamati hiyo imewataka wanachama wake kupitia maoni ya wananchi ambao alidai wamepoteza imani na Ukawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles