30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MUFTI: WAISLAMU ANZENI KUJIANDIKISHA HIJJA

Na PATRICIA KIMELEMETA – Dar es Salaam


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limetangaza msimu wa Hijja na kuwataka Waislamu wanaotaka kwenda Makka kuhiji kuanza kujiandikisha kuanzia sasa hadi Aprili 10, kwa gharama ya Dola za Marekani 3,700 hadi 4,700.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari bin Zuberi, alisema ili kuhakikisha uandikishaji huo unafanyika kwa wakati, baraza limepitisha taasisi 15 kusajili na kusafirisha mahujaji, huku taasisi ya Al-Madina ikizuiliwa kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema Waislamu wenye uwezo wanapaswa kujiandikisha kwenye taasisi hizo ili waweze kwenda Makka kukamilisha ya nguzo ya tano ya Kiislamu.

“Naomba taasisi zote zilizopitishwa kusafirisha mahujaji mwaka huu zifanye kazi kwa uadilifu na kuondoa mianya yote ya utapeli ili kuepusha usumbufu,” alisema Mufti Zuberi.

Alisema kutokana na hali hiyo, taasisi hizo zitazingatia muda uliopangwa kusajili na kulipia gharama ili ifikapo Mei 16, zoezi hilo liweze kufungwa.

Mufti alisema mwaka huu, Serikali ya Saudia imetoa nafasi za watu 26,000 kwenda kuhiji, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Mwaka jana tulisafirisha mahujaji 2,700 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wakati nafasi tulizopewa ni mahujaji 15,000. Mwaka huu wameongeza hadi kufikia nafasi 26,000, ni wakati wa kuhamasisha Waislamu kujitokeza kwa wingi ili kwendakuhiji Makka,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Hamis Mattaka, alisema kuna taasisi ambazo zilijitokeza mwaka jana kusafirisha mahujaji, lakini zilishindwa kufanya hivyo, na wahusika wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kwa kosa la utapeli.

Alisema taasisi hizo ziliingia mkataba wa kuwalipa mahujaji hao baada ya kushindwa kuwasafirisha, lakini hadi sasa wameshindwa kurudisha fedha hizo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Uhamiaji, Gerald Kihingo, alisema mahujaji wanapaswa kushughulikia utaratibu wa paspoti mapema ili kuondoa usumbufu.

“Kwa wale wenye paspoti za zamani wanaweza kuzitumia, lakini kwa wale ambao hawana wanaweza kufika kwenye ofisi za Uhamiaji au kutumia taasisi walizojiandikishia kufuata utaratibu wa utoaji wa paspoti,” alisema Kihingo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles