KIGALI, RWANDA
MARUFUKU ya matumizi ya adhana, ambao ni wito kwa Waislamu kuhudhuria ibada msikitini katika tarafa moja ya mji wa Kigali nchini Rwanda imepingwa vikali na baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu jijini humo.
Utawala katika tarafa ya Nyarugenge kunakopatikana jamii kubwa ya Waislam nchini humo umebainisha kuwa kumekuwepo muafaka wa kubadili mbinu za kuwaita waumini bila ya matumizi ya njia hiyo ambayo inatajwa kuwasumbua wananchi.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mjini Kigali, John Gakuba wito huo wa Waislamu kuhudhuria maombi umetajwa kuwa kero miongoni mwa wananchi.
Tayari mkataba wa kuhakikisha kuwa mwafaka huo unaheshimiwa umetiwa saini kati ya viongozi wa msikiti na utawala wa eneo hilo.
Wito huo wa maombi miongoni mwa jamii za Waislamu kote duniani hutumia vipaza sauti na hufanyika mara tano kwa siku.
Licha ya utawala wa eneo hilo kudai kwamba kumekuwa na mwafaka kutoka pande zote mbili baadhi ya Waislamu waliohojiwa wametoa hisia tofauti.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa tarafa hiyo, amri hiyo iliagizwa yapata miaka miwili iliyopita lakini ikapuuzwa.
“Wakati ule watu hawakupokea vyema ujumbe lakini leo baadhi ya makanisa yalilazimika kufunga milango baada ya kushindwa kutimiza kanuni za ujenzi huku misikiti yenye vipaza sauti na makanisa yenye kengele tukiyataka kutotumia mtindo huo,” alisema.