29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda amtaja Lowassa

PINDANa Debora Sanja, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, jana amechukua fomu ya kuwania urais, huku akieleza rekodi alizoziweka tangu alipochukua nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Edward Lowassa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma, Pinda, pamoja na mambo mengine, alieleza mambo aliyoyafanya kuwa ni pamoja na kuendeleza yale aliyoyaasisi mtangulizi wake huyo.
Pinda alimsifia Lowassa kwa kusimamia mchakato wa ujenzi wa shule za sekondari nchini ambapo sasa kuna ongezeko la shule za sekondari za kata zaidi ya 4,000.
“Hili pia la ongezeko la sekondari hamlioni, tunamshukuru Edward, alijitahidi kwa miaka miwili yakamkuta yaliyomkuta, lakini kama tungesema haya ya Edward tusingeyaendeleza,” alisema Pinda.
Wakati Pinda akisema hayo, hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, alikaririwa na chombo kimoja cha habari (si MTANZANIA Jumamosi) bila kutaja jina la mtu akibeza wanaojisifu kwa shule za sekondari za kata.
Si yeye tu. Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakati akitangaza nia ya kugombea urais naye alizungumza jambo hilo hilo kwa namna ya kukosoa.
Mbali na hilo, Pinda, ambaye alikuwa akijibu swali juu ya mambo mapya ambayo atayafanya, licha ya kuongoza serikali kwa muda mrefu na zaidi ikigubikwa na ubadhirifu, alisema amefanya mengi, lakini hana desturi ya kujisifia, huku akijivuna kuwa na baraza la mawaziri imara.
“Mimi nipo Serikali za Mitaa tangu nilipoingia kwenye siasa, CAG mweyewe (Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali) anatusifia katika kaguzi zake tofauti na miaka ya nyuma ambapo hali ilikuwa ni mbaya.
“Hadi sasa tumeshafukuza wakurugenzi watendaji zaidi ya 2,000, bahati mbaya tu mie sina tabia ya kujisifu.
“Na kama unadhani huyo ambaye hakuwemo madarakani ndo atakuja na kitu kipya umefanya kosa, kwa kuwa akija ataanza kwanza kujifunza, aelewe na mwisho ataboronga tu.
“Simba mwenda pole ndiye mla nyama nono, tazama hata mawaziri wangu wanavyofanya mambo mazuri, alikuja Muhongo akaondoka (Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini), mtazame Magufuli (Dk, John Magufuli, Waziri wa Ujenzi), mkiwaona hawa jueni kiranja wao ni mimi,” alisema Pinda, ambaye hata hivyo alisema anayemjua rais ni Mungu.
Aliwataka Watanzania kutokufanya maamuzi yasiyo sahihi kuhusu yeye halafu baadaye wakayajutia.
“Nimeyasimamia yote haya, lakini bahati mbaya tu majigambo sina, la sivyo ningekuwa mtu wa makeke, mbona mngenikoma,” alisema.
Kuhusu kauli yake aliyowahi kunukuliwa kwamba hautaki urais na kwamba amejiandaa kustaafu kwenda kufuga nyuki, Pinda alisema ni kweli wakati alipotoa kauli hiyo mwaka 2012 hakuwa na ndoto ya urais.
Alisema wakati ule suala halikuwa urais, lakini aliwaambia wapiga kura wake kwamba miaka 15 ya kuwa mbunge wao inatosha na kwamba hatagombea tena nafasi hiyo.
“Lakini hata kama ningekuwa nimesema hivyo hakuna ubaya, wakati ule ilikuwa mwaka 2012, hivyo nikibadili msimamo wangu kuna tatizo gani? Hata mke ukimuacha unaweza ukamrudia.
“Binadamu ndivyo tulivyoumbwa na kama tungekuwa tunakata tamaa basi tena, lakini baadaye unapata nguvu mpya, msukumo mwingine, ushawishi kutoka kwa ndugu, marafiki na hata Mwenyezi Mungu.
“Hata hivyo, siku zote huwa nasema urais ni jambo kubwa na mimi nimeamua kujitosa katika hili, lakini hata kama nikipata iwe ni kwa mapenzi yake Mungu,” alisema.
Pinda alisema hawezi kusema lolote kuhusu mambo atakayoyafanya, lakini ana uhakika hawezi kushindwa kutekeleza Ilani ya CCM itakayopitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho.
“Ilani yetu bado haijatoka, humo ndipo kutakuwepo na sera, maelezo na mikakati yote, kwa hiyo sina cha kusema mpaka ilani itakapopitishwa na ikitokea nikateuliwa sitashindwa kuitekeleza na nalisema hili kwa uhakika,” alisema.
Pinda alisema amefanya kazi na marais wa awamu zote, amejifunza mengi na kwamba amekuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka minane, akiwa ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Alisema Rais Jakaya Kikwete amefanya mambo mengi, ikiwemo kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoishia mwaka 2025, dira iliyoasisiwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Alisema dira hiyo inatekelezwa katika kipindi cha miaka mitanomitano na kwamba Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano ya awali unaishia mwakani.
“Sasa katika miaka mitano inayokuja ni kwa ajili ya kujenga uwezo wa kiuchumi kwa kujenga viwanda vya kusindika mazao yanayotokana na mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi,” alisema.
Alisema uchumi wa Watanzania unakua, lakini bado Watanzania ni masikini kwa kuwa uchumi huo unakua kwa kutegemea sekta ya ujenzi, maliasili na uchukuzi, sekta ambazo haziwagusi watu wengi.
“Kwa hiyo katika mpango wa miaka mingine mitano, tutajikita kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, tukifanya hivi umasikini utapungua kwa kiwango kikubwa na ajira zitapatikana.
“Kama ikimpendeza Mwenyezi Mungu, hili ni eneo ambalo piga geuza, nitaelekeza nguvu zangu hapo,” alisema Pinda.
Aidha, iwapo atafanikiwa kuwa rais, badala ya kupambana na maadui watatu ambao ni umasikini, ujinga na maradhi, yeye ataongeza maadui wawili ambao ni uharibifu wa mazingira na utawala bora.
“Watanzania wote tunawajibika kuhakikisha nchi inaongozwa kwa uwazi na kuwa na viongozi wenye maadili ambao wana uchungu na umasikini wa Watanzania.
“Tutaangalia jinsi ya kuipa meno TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), kama si mla rushwa hakuna haja ya kuogopa hili, mtu akikamatwa apelekwe mahakamani, hakuna hata haja ya kuomba kibali kwa Waziri Mkuu.
“Uchungu wa mwana aujuaye mzazi, mimi ndiye nipo serikalini kwa sasa, kwa hiyo kama ni uchungu wa mwana, mimi ndiye ninayeujua kwa sasa,” alisema.
Pinda alichukua muda pia kuwashukuru viongozi wote wa kitaifa, akiwemo Rais Jakaya Kiwete, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Wengine ni viongozi wa chama wa ngazi zote, viongozi wa vyama vya siasa, vyama visivyo vya kiserikali na viongozi wa ngazi zote za serikali za mitaa, wakiwemo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, mameya, madiwani na watendaji wengine.
Baadhi ya watu waliomsindikiza Pinda kuchukua fomu ni pamoja na mwanasiasa mkongwe aliyekuwepo katika Baraza la Mawaziri la Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Job Lusinde na aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya awamu ya tatu, Dk. Chrisant Mzindakaya.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria halfa hiyo ni pamoja na Mbunge wa Manyovu, Obama Ntabaliba, Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Pudencia Kikwembe, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata na Mbunge wa Mbarali, Moshi Kakoso.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles