29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

NICOL YAIMARIKA, YASUBIRI KURUDI SOKO LA HISA DAR ES SALAAM 

Na Shermarx Ngahemera


KAMPUNI ya Taifa ya Uwekezaji (NICOL)  ya wazalendo imepitia  majaribu makubwa  na sasa imeanza  kupata faida baada ya kupata uongozi mpya na imeanza kutoa gawio kwa wanahisa wake baada ya miaka takriban zaidi ya 10 ya sintofahamu na vuta nikuvute.

NICOL ni kampuni ya kizalendo ilianzishwa kwa ushirikiano wa karibu  baina ya Serikali na vyombo vyake, pamoja na viongozi mbalimbali, wabunge na wananchi ili kuhamasisha  uwekezaji kwa  wazalendo na hivyo kupata tokea mwanzo mwitikio mkubwa kutoka kwa watu  wengi  kununua hisa.

Hadi sasa NICOL ni kampuni pekee ya kizalendo yenye uzito mkubwa  wa uwekezaji  na mtaji mkubwa  kushinda  makampuni yote ya kizalendo (collective investment scheme).

Pamoja na changamoto nyingi za awali za kiuongozi hali ya kampuni sasa imeimarika  baada ya wanahisa  kuweka uongozi mpya madarakani na faida kupatikana na kampuni kuanza kutoa gawio kwa wanahisa wake.

Nilipomwuliza Dk Gideon Kaunda, Mwenyekiti wa NICOL katika mahojiano mahsusi  ofisini kwake  alisema kwa kujiamini kuwa mambo ni shwari na hiyo inathibitishwa na kampuni hiyo kushinda kesi zote 43 za kupandikiza zilizokuwa zimetengenezwa na utawala king’ang’anizi uliopita ambao ulijitahidi kuhujumu kampuni hiyo kwa mengi ili usitoke madarakani.

Anasema masahibu ya hujuma kwa kampuni ya NICOL  yameainishwa  vilivyo katika Ripoti yake ya mwaka 2016 ambayo inalaani uongozi uliopita kwa kukosa weledi na uzalendo kwenye mambo mengi.

Anasema kampuni  ya NICOL pamoja na kuhujumiwa na kuwa kimya kwa miaka 13  bila kutoa gawio imeweza kufanya kazi na kupata faida na sasa mtaji wake ni zaidi ya shilingi bilioni 100 na inatafuta mahala  pazuri pa kuwekeza kwa kupanua wigo wake.

Anasema tokea awe kiongozi wa NICOL ameweka juhudi yake zaidi kwenye utawala bora na uwekezaji wenye tija ambao sasa matunda yake yameanza kuonekana.

“Tumeweza kutayarisha na kufanya mahesabu ya Kampuni  kutokea 2009  na kwa mwaka 2016 na hivyo kuweza kufanya mkutano tarehe 2 Disemba mwaka jana (2017 ) ambapo  wanahisa 600 walihudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka ingawa uongozi uliotangulia uliweka pingamizi  la mkutano huo  usifanyike lakini Mahakama  ilitupilia mbali kutokana na kukosa sababu ya msingi .”

Kutaka kurudi DSE

Dk Kaunda  anasema lengo la kwanza ni kurudi kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambako kampuni iliwahi kusimamishwa mwaka 2011 kufuatia Menejimenti ya NICOL kushindwa kufuata masharti ya lazima ya kuendelea kuweko kwenye Orodha ya DSE (Continuing Listing Obligations ) kwa kufanya  kwa kificho maamuzi mengi  muhimu  ya uwekezaji yakiwemo  manunuzi na mauzo  bila kuishirikisha DSE na bodi ya Wakurugenzi wa NICOL na hivyo kuwa batili.

Matendo hayo ni kinyume cha taratibu na kanuni za miongozo ya Soko la DSE na hivyo Kampuni kupoteza fedha nyingi kutokana na kukosa kuzingatia mwenendo sahihi wa uendeshaji kampuni ya umma (plc) kama NICOL na hivyo kutumbukia katika lindi la madeni  kwa wakati fulani yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 11.5 ingawa kwa sasa madeni hayo yamelipwa na uongozi mpya.

Anasema mambo ni moto moto kwa bodi mpya.

Bodi mpya chini ya Dk Kaunda  anasaidiwa na wajumbe Joyce N. Nyanza  na Mhandisi Ladislaus Salema na Mwanasheria Benjamin Mwakagamba.

“Kazi yetu ya kwanza ilikuwa ni kuinusuru kampuni kutokana na matishio mbalimbali   ya kisheria na kiutawala kitu ambacho  kampuni imefanikiwa kwa kushinda kesi  zote 43 mahakamani , imelipa madeni na hakuna kesi iliyobakia  na sasa mambo ni shwari na hivyo tumeanza kutoa gawio kwa wanahisa wetu,” anaeleza Dk Kaunda.

Ripoti hiyo ya mwaka 2016 yenye kurasa 80 imeeleza kwa marefu na mapana mwenendo wa Uongozi uliopita na ubadhirifu uliofanyika na mwishowe mahakama kuutupilia mbali nje ya kampuni.

Matendo ya uongozi uliopita ulifedhehesha sana mwenendo wa NICOL na kitendo cha Mahakama Kuu kufukuza na kupiga marafuku wale wote waliohujumu NICOL ni matendo yaliyopongezwa na wote wapenda maendeleo ya haki kwenye Mkutano Mkuu mwaka jana.

Mwaka jana NICOL imedai kupata faida ya shilingi bilioni 8.67/- baada ya kodi na kutoa gawio la shilingi 252/- kwa hisa kwa kampuni ambayo ilianza mwaka 2004 na wanachama  wenye hisa 148 na mtaji wa shilingi milioni 140/- . Kampuni ina mtaji ulioidhinishwa wa shilingi Bilioni 200  na kugawanywa kwenye hisa bilioni 1.6 kwa bei ya shilingi 125 kwa kila hisa.

Mwenyekiti Kaunda anatoa ahadi ya kulipa gawio kila mwaka kuanzia sasa kwani biashara ni nzuri hasa wakati huu ambapo nchi ina mipango ya uchumi wa viwanda na hivyo kufungua milango ya uwekezaji  mpya kwa marefu na mapana.

Anasema, Kampuni ina rasilimali za kutosha kwani ina hisa katika makampuni  tisa  makubwa  zenye thamani isiyopungua shilingi bilioni 100/- wakati wana amana yao Benki Kuu  ambayo iko hapo kuanzia mwaka 2011 na haijaguswa. Makampuni hayo yahaja yanayofanya shughuli zake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ni Benki za NMB, CRDB, Tanzania Breweries, Swissport, Simba Cement, Twiga Cement, Vodacom, TCC na DSE.

“Kampuni  nayo iliwahi kuwekeza kwenye vitalu huko Mtwara na vimetengeneza faida na katika benki ya NMB Kampuni ina umiliki wa asilimia 6.6 na asilimia 3.3 hisa za DSE,” anafichua Mwenyekiti.

Anasema Dk Kaunda  kuwa kimsingi ukiachia mambo ya hujuma zilizofanywa na uongozi uliopita uwekezaji wa NICOL ulikuwa mzuri  na wa kimkakati kwani uwekezaji kwenye benki, vitalu, viwanda viwili vya kuchakata nyama ya ng’ombe na mbuzi  na  kiwanda cha kuchakata samaki vyote vilianza vizuri lakini uongozi uliokuwepo  wakati huo ulivuruga  na kuleta sintofahamu  nyingi  kwa vitendo vyake  vilivyokosa  uwazi, uaminifu kwenye masuala mbalimbali  yanayohusu kampuni ya NICOL.

Dk Kaunda anasema mara nyingi  vitendo  viovu kama vilivyoonekana kwenye  kesi  43 mbalimbali viliweza  kuathiri na kutishia  ustawi  wa  kampuni kutokana na kukithiri matendo ya kulana kisogo, kukosa uaminifu, ustadi  na kukosa weledi wa kitaaluma  wa uendeshaji mambo. Lakini  hiyo ni historia kwa sasa na hivyo anawakaribisha watu wote kununua hisa za NICOL pale ambapo tangazo litakapotoka  la kurudishwa tena Sokoni.

“Hali ya kifedha ni nzuri  baada ya  kulipa kodi  ya Serikali pamoja na malimbikizo mbalimbali ya madeni na hivi sasa tuko tunafuatilia mambo ya uwekezaji ili tukirudishwa sokoni shughuli zianze kwa kwenda shoti.”

Anasema pamoja na Matatizo yote waliyopitia wanaendelea kuhakikisha  mtaji wa NICOL unaimarika ili kuleta maendeleo na mafanikio  makubwa kwa wanahisa katika siku za usoni.

Mwenyekiti anasema Kampuni imekatishwa  tamaa na maamuzi mengine  ya mikataba ya kitapeli ambayo yameifanya baadhi ya miradi kuchukuliwa na wapangaji wao na NICOL kubakia kama mchinjaji wa nyama badala ya kuwa mwuzaji wa nyama katika viwanda vyake anavyomiliki.

“Viwanda vya nyama  vya Tanzania Meats Company (TMC) na East Africa Meat company vinauwezo wa kuchinja ng’ombe 300 na mbuzi 500 kwa siku  na kuuzwa Irak na Vietnam lakini kasoro kubwa ni kuwa mauzo  hayo yalifanyika kwa fedha tasilimu (cash) na hivyo hakuna taarifa rasmi ya hujuma hiyo kwani biashara inafanywa na kampuni tanzu ya Ako. Kwa vile Nicol ni kampuni ya Umma imeanzisha  Ukaguzi wa kijinai (forensic audit) ili kuchunguza  kwa kina mwenendo mzima  wa uendeshaji wa kampuni na hasara zilizopatikana  ili kutambua nafasi ya kila mhusika katika kusababisha hasara ya fedha na kuipaka matope kampuni  kwa kuhisiwa kuwa na mwenendo mbaya wakati ni matendo ya watu binafsi na sio kampuni husika.

Hali hiyo inaonesha kipato cha NICOL ni kidogo wakati biashara ni nzuri na ya faida kubwa na kuiweka kampuni katika nafasi nzuri.

Lakini Mwenyekiti Kaunda anajulikana katika utendaji na usimamizi mzuri  wa miradi kwani mwaka 1995 hadi 2000 aliweza kuanzisha na kuendesha ‘Alliance Air’ ambayo ilikuwa ina ndege zilizokodishwa na Air Tanzania na ilikuwa inaiingizia faida serikali kiasi cha Dola milioni 30 kwa mwaka.

Walipokuja Shirika la Ndege la Afrika ya Kusini (SAA) walipata hasara hadi walipoondolewa kwa kushindwa kujiendesha kibiashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles