Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Serikali imezitambua dawa tano zilizotengenezwa kiasili ikiwamo dawa ya ujana ambayo inadaiwa ina uwezo wa kuongeza nguvu za kiume baada ya kuthibitisha ubora na usalama wa dawa hizo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile amesema dawa hiyo pamoja na nyingine zimethibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Amezitaja dawa nyingine kuwa ni IH Myoon, Colloidal Silver, Sudhi na Vatari ambazo zinadaiwa kutibu magonjwa mbalimbali ambapo pia amesema dawa hizo zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
“Tatizo la upungufu wa nguvu za kiume lipo dunia nzima, Tanzania bado hatujafanya utafiti kujua lipo kwa kiasi gani, linachangiwa na mambo mengi hasa ulaji mbovu, kutokufanya mazoezi, uvutaji wa sigara, unywaji pombe na hata ulaji wa nyama za kuku waliozalishwa kwa kuongeza homoni,” amesema.
Aidha, Dk. Ndugulile ametoa onyo kwa vyama vya waganga wa tiba asili na tiba mbadala ambao wanapita kwa waganga na kuwasajili jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.
“Wenye mamlaka ya kusajili ni Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lakini pia vyombo vya habari ni marufuku kutoa matangazo ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala ambayo hayajasajiliwa, vikiwamo vipindi vya redio na televisheni, tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza hilo, Dk. Ruth Suza amesema dawa hizo zimesajiliwa na kutambulika baada ya kuhakikiwa ubora wake katika Kitengo cha Botany cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Ofisi ya Mkemia Mkuu.
“Zimeonekana kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu, lakini kuhusu kutibu huko tunakoelekea tutaangalia uwezo wake wa kutibu sasa hivi tunazipima ubora wake zinapokwenda kwenye jamii ni salama kwa afya au la,” amesema Dk. Suza.