CHRISTINA GAULUHANGA Na REHEMA JUMA (RCT) -DAR E SALAAM
UTAFITI uliofanywa nchini katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara umebaini asilimia 38 ya watoto wenye umri wa miaka tisa hadi 13, hawawezi kufanya majaribio ya masomo ya darasa la pili.
Akizungumzia katika mjadala wa utafiti uliofanywa na kitengo cha Uwezo Tanzania chini ya Taasisi ya Twaweza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema, utafiti huo ulionesha tofauti kubwa ya ufanyaji majaribio kwenye wilaya mbalimbali.
Alisema Wilaya ya Iringa Mjini imebainika inaongoza kwa ufaulu kwa asilimia 75 ya watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13 wenye uwezo wa kufanya majaribio ya Kiingereza ,Kiswahili na hesabu za darasa la pili.
“Cha kushangaza wilayani Songwe ni asilimia 17 tu ya watoto walioweza kufaulu majaribio hayo,”alisema Eyakuze.
Eyakuze alisema asilimia 64 ya watoto mkoani Dar es Salaam wenye miaka tisa hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio hayo matatu lakini mkoani Katavi ni asilimia 23 tu wanaofaulu majaribio hayo.
Pia watoto wawili kati ya kumi wenye umri wa miaka 11 sawa na asilimia 16 wa Mkoa wa Dar es Salaam wako nyuma kimasomo ambapo idadi hiyo mkoani Katavi ni watoto saba kati ya kumi.
“Takwimu hizi zinaonesha maeneo wanapoishi watoto yana mchango mkubwa katika kujifunza kwa watoto hao kuliko umaskini, kiwango cha elimu ya mama, iwapo mtoto amesoma shule ya awali au hata wenye udumavu,”alisema Eyakuze.
Alisema matokeo hayo yamepatikana kwenye ripoti ya Uwezo Tanzania ya mwaka 2017 iitwayo Je, Watoto wetu Wanajifunza? Na Upimaji wa kujifunza.
Alisisitiza kuwa ripoti hiyo inatokana na takwimu zilizokusanywa na Uwezo, tathimini kubwa barani Afrika ya kupima matokeo ya kujifunza nchini Kenya, Tanzania na Uganda.
Eyakuze alisema katika awamu ya sita ya ukusanyaji takwimu uliofanywa na kitengo hicho mwaka 2015 jumla ya watoto 197,451 walitathiminiwa kutoka kaya 68,588 ambapo takwimu zilikusanywa katika shule za msingi 4,750.
“Tofauti kubwa zilibainika pia katika vifaa, rasilimali na huduma zipatikanazo shuleni,” alisema Eyakuze.
Alisema utafiti huo ulibaini pia mkoani Dar es Salaam asilimia 51 ya nusu ya shule zina huduma ya umeme wakati mkoani Geita ni shule mbili kati ya 50 sawa na asilimia nne zinazopata huduma hizo.
Inaendelea………………. Jipatie nakala yako ya gazeti #MTANZANIA