ABUJA, NIGERIA
SERIKALI ya Nigeria imesema imeongeza ndege ya kivita katika operesheni ya kuwatafuta wanafunzi wa kike waliotekwa Kaskazini Mashariki mwa nchi hii.
Takriban wasichana 110 wanaelezwa hawajulikani walipo baada ya wanamgambo wa kundi la Boko Haram kuwateka katika shule yao iliyopo Dapchi.
Mapema Serikali ya Kijiji cha Dapchi ilililaumu jeshi kwa kushindwa kuchukua hatua hata baada ya kupewa taarifa.
Hasira zimekuwa zikiwapanda wazazi wa wasichana hao, huku kukiwa na ripoti kuwa wanajeshi walikuwa wameondolewa kutoka kwenye vizuizi vikuu vya Dapchi mwezi uliopita.
Dapchi ambao ni mji ulio kilomita 275 kaskazini magharibi mwa Chibok, ulishambuliwa Jumatatu iliyopita na kusababisha wanafunzi na walimu kutoka shule moja ya Serikali kukimbilia vichakani.
Wenyeji wanasema vikosi vya Jeshi la Nigeria vikisaidiwa na ndege za vita baadaye vilizima uvamizi huo.
Awali mamlaka zilikana kuwa wasichana hao walikuwa wametekwa, zikisema walikuwa wamejificha.
Lakini baadaye mamlaka zilikiri kuwa wasichana 110 walikuwa hawajulikani waliko baada ya uvamizi huo.
Hatua ya kutekwa nyara kwa wasichana hao, imeibua maswali kuhusu tamko la mara kwa mara la Jeshi la Nigeria, kwamba kundi la Boko Haram linaelekea kuangamizwa baada ya miaka tisa ya kupambana nalo vikali.
Utekaji huo umezifufua kumbukumbu za mwaka 2014 wakati zaidi ya wasichana 200 wa shule walitekwa nyara eneo la Chibok.
Siku ya Ijumaa, Rais Muhammadu Buhari aliziomba radhi familia za wasichana waliotoweka akisema ni janga la kitaifa.