26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

IGP: TUMEPATA TAARIFA YA MAANDAMANO NCHI NZIMA

NA SAMWEL MWANGA – SIMIYU


MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, ametoa onyo kali kwa wanasiasa ambao wamepanga kuandamana nchi nzima.

Amesisitiza jeshi hilo limejipanga vizuri kukabiliana nao.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bariadi mkoani Simiyu jana, IGP Sirro alisema jeshi hilo limepata taarifa kutoka vyanzo vyake kuna makundi ya vijana wanaojiita Wana Mapinduzi, wamepanga kuandamana nchi nzima.

Alidai kuwa vijana hao wamepanga kuandamana chini ya uratibu wa chama kimoja cha siasa ambacho hakukitaja kwa jina.

Alisema kutokana na taarifa hiyo, wamejipanga kuwakamata watu wote watakaojaribu kuandamana na kwamba hayuko tayari kuona hali ya amani inavurugwa.

“Tumepata taarifa kuna vijana wanajipanga kuandamana nchi nzima, nawaambia polisi tumejipanga vyema kuhakikisha tunawadhibiti

wasiweze kufanya chochote. Mtu yeyote ambaye atajaribu tutamchukulia hatua kali za kisheria.

“Kama unataka usumbufu utacheza na Sirro, sasa hivi wanasema wamejaza mamia kwenye mitandao eti wapo na wanaendelea, nasisitiza nafasi hii hawataipata hata kidogo,” alisema IGP Sirro.

Kutokana na hali hiyo, aliwatahadharisha wazazi na walezi kuwaonya vijana wao wanaotaka kuandamana kuacha mpango huo kwa sababu jeshi hilo halitakuwa na huruma na mtu yeyote.

Kuhusu hali ya uhalifu, IGP Sirro alisema jeshi hilo limeweza kuudhibiti katika maeneo mengi ya nchini, hasa wa kutumia silaha  na wizi mdogo mdogo wa vijana ambao wamekosa malezi mazuri kutoka kwa wazazi wao.

“Kuvunja sheria ni rahisi, madhara yake ni makubwa, wananchi wajitahidi kufanya kazi na wasijiingize kwenye tamaa ambazo baadaye zinaweza kukugharimu maisha yako,” alisisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, akitoa taarifa ya usalama kwa mkoa wake, alisema hivi sasa hauna matukio makubwa ambayo miaka ya nyuma yalikuwapo kama ya mauaji ya vikongwe na albino.

Alisema changamoto kubwa  inayowakabili askari ni uhaba wa nyumba za makazi na kumwomba IGP katika  bajeti ijayo waiangalie Simiyu juu ya ujenzi wa nyumba kupunguza wimbi la askari kuishi uraiani.

“Tunakabiliwa na changamoto kubwa ya makazi ya askari,  wengi wamepanga uraiani, wakati  mwingine ni vigumu kufanya kazi kwani mazoea kati yao na raia yakizidi, hawawezi kufanya kazi kwa weledi, tunaomba bajeti ijayo ya Serikali muone namna ya kutusaidia,” alisema Mtaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles