31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

WANASHERIA WAHAHA KUMNUSURU SUGU

Na PENDO FUNDISHA – MBEYA


MAWAKILI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanahaha kumuokoa kifungoni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina Sungu (Chadema), aliyehukumiwa jana kwenda jela kwa miezi mitano.

Msimamo huo ulitolewa jana na Mawakili wa Chadema, Profesa Abdallah Safari na Peter Kibatala, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari baada ya hukumu hiyo.

“Tutakata rufaa kwa sababu hatukuridhishwa na hukumu dhidi ya mbunge wetu pamoja na Katibu Masonga,” alisema Profesa Safari.

Kama alivyosema Profesa Safari, Wakili Kibatala naye alisema hawakuridhika na hukumu kutokana na sababu tisa walizonazo.

Kwa mujibu wa Kibatala, jana hiyo walikuwa wamewasilisha maombi mawili ya kukata rufaa katika mahakama ya juu na kuomba dhamana ya mbunge huyo.

Sugu na Masonga walihukumiwa bila faini baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya kutoa lugha za fedheha dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Mbeya, Michael Mteite, alisema mahakama iliwatia hatiani watuhumiwa baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa Hakimu Mteite, ushahidi huo ulikuwa wa kuona na kusikia na ulitolewa na mashahidi watatu.

Shahidi wa nne ambaye ni Inspekta wa Polisi, Joram Magova, alitoa ushahidi wa sauti iliyorekodiwa.

Katika mashtaka hayo, Sugu na Masonga walidaiwa kutoa maneno hayo Desemba 30, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge ya jijini Mbeya.

Hata hivyo, katika utetezi wake, Masonga alisema hakuwapo mkutanoni hapo siku hiyo kwa kuwa alikuwa nyumbani kwake akimuuguza mkewe.

Akisoma mwenendo wa kesi kabla ya hukumu, Hakimu Mteite alisema wakati ushahidi ukiendelea, mmoja wa mawakili wa washtakiwa, Boniface Mabukusi, alipinga mahakama kupokea ushahidi wa sauti uliorekodiwa kwa kuwa haukuwa na maana.

Pia, mawakili hao walipinga kupokewa kwa kitabu cha kumbukumbu kilichotolewa na shahidi wa upande wa mashtaka ambaye ni askari polisi, Daniel Masanja.

Pamoja na hayo, Wakili Peter Kibatala aliyekuwa miongoni mwa mawakili hao wa utetezi, alipinga hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani hapo kwa kutoonyesha nani mlalamikaji halali wa shauri hilo.

Pia, alisema shahidi wa pili wa upande wa utetezi ambaye ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya (OCD), James Chacha, alionekana kutetereka wakati akitoa ushahidi wake.

Wakati huo huo, Wakili Kibatala alitaka mahakama isipokee ushahidi wa mashahidi wawili ambao ni shahidi wa tatu, Inspekta wa Polisi, Willium Nyamakomagu na shahidi wa nne, Inspekta Joram Magova.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo, Hakimu Mteite alisema mahakama hiyo ilipokea ushahidi wa mashahidi hao kwa kuwa waliidhihirishia kwamba walikuwapo kwenye mkutano na waliona na kusikia kilichokuwa kikizungumzwa na washtakiwa.

Hakimu Mteite, aliendelea kufafanua kuwa mahakama pia ilijiridhisha kwa kuangalia maneno yaliyotamkwa na washtakiwa kama yalibeba ujumbe wa fedheha na yalimlenga Rais Magufuli.

“Ukiangalia mashahidi wote waliotoa ushahidi kwa upande wa mashtaka, utaona jinsi walivyoeleza kwamba aliyetolewa maneno hayo ya fedheha ni Rais.

“Pia, mahakama ilijiridhisha kwamba mkutano huo ulikuwa ni wa kisiasa na aliyekuwa akizungumza ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya ambaye ni mwakilishi wa wananchi.

“Tanzania ina mtawala mmoja ambaye ni Rais John Magufuli, hivyo ujumbe huo ulilenga moja kwa moja kwake na si Magufuli mwingine kama ilivyoelezwa na Wakili Kibatala wakati akiwatetea wateja wake.

“Pia, ikumbukwe kwamba kiongozi anayeweza kutatua changamoto za kitaifa ni Rais Magufuli peke yake na huo mkutano ulikuwa ukieleza shughuli za maendeleo na kujadili mustakabali wa taifa kama ilivyoelezwa na shahidi wa tano wa upande wa utetezi, Boid Mwabulanga.

“Lakini pia, siyo kila kesi hasa za Serikali, lazima mlalamikaji asimame mahakamani kama ilivyoelezwa na Wakili Mabukusi alipokuwa akimhoji shahidi wa pili ambaye ni OCD.

“Kwa ujumla, kesi hii ilifunguliwa na Serikali kwa sababu aliyekashfiwa ni rais ambaye ana majukumu mengi na hawezi kusimama mahakamani, hivyo hii haikuwa sababu ya kutaka kesi hii isisikilizwe,” alisema Hakimu Mteite.

Awali kabla ya hukumu, Wakili wa Serikali, Joseph Pande, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa kwa kuwa walimkashfu Rais na maneno yao yalionyesha kuhatarisha amani ya nchi.

Kwa upande wake, Wakili Kibatala aliiomba mahakama ikumbuke washtakiwa walikuwa wameshatumikia mwezi mmoja mahabusu baada ya kukosa dhamana Januari 16, mwaka huu hadi Februari 8, mwaka huu walipodhaminiwa.

Pia, aliiomba mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa pasipo uvunjifu wa amani au kutoa adhabu nyingine yoyote au ya miezi sita jela.

Pamoja na hayo, Wakili Kibatala alisema ndoa za washtakiwa ni changa na wana watoto wanaowategemea, hivyo mahakama ione jinsi ya kuwapunguzia adhabu.

Pamoja na utetezi huo, Hakimu Mteite, aliwahukumu watuhumiwa hao kwenda jela miezi mitano bila faini.

Kesi hiyo ilisomwa kwa mara ya kwanza Januari 16, mwaka huu na watuhumiwa kupelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana hadi Februari 8, mwaka huu.

Katika shauri hilo, Sugu alidaiwa kusema kwamba kama Rais anataka kupendwa na asingemshuti Lissu, asingemfunga Lema miezi minne gerezani, asingemzuia yeye Sugu asiongee hili au lile kwa kuteka watu.

Kwa upande wa Masonga, alidaiwa kusema hali ya maisha imekuwa ngumu, kila kona mambo yamekaza, watu wanatekwa mchana kweupe, watu wanauawa na kufungwa kwenye viroba mchana kweupe.

Katika hatua nyingine, ulinzi mahakamani hapo jana uliimarishwa kwa idadi kubwa ya polisi.

Sugu na Masonga ambao walikuwa nje kwa dhamana, walifika mapema mahakamani hapo kabla ya kuanza kusomwa kwa kesi hiyo, saa 3:30 asubuhi.

Baada ya Sugu na Masonga kuingia eneo la mahakamani, askari polisi walitanda kila kona ya mahakama, huku wakiwataka wanachama wa Chadema kutoingia kusikiliza kesi ya viongozi wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles