27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MFUNDISHE MTOTO KILE UNACHOKIAMINI


Na Christian Bwaya

NAKUMBUKA nikiwa na umri wa miaka kama mitano na kuendelea baba yangu alikuwa na utaratibu tuliouchukulia kama desturi ya nyumbani. Kila jioni, baada ya michezo mingi ya siku, ilikuwa ni sharti mimi na wadogo zangu wawili tukutane naye sebuleni kufanya ibada ya pamoja. Katika ibada hizo, tuliimba, tulisali, na kusikiliza hadithi zilizotokana na mafundisho ya biblia.

Hadithi ndiyo sehemu iliyotuvutia zaidi sisi watoto. Tulivutiwa na hadithi kiasi kwamba hata kama tungejua baba alikuwa hajarudi nyumbani siku hiyo, bado tungeliwahi nafasi za kukaa tukiwa na majirani kumsubiri baba afike kuendelea pale tulipoishia jana.

Mzee alitumia hadithi kutufundisha mambo mengi yanayohusu imani na maadili. Kipindi hicho, miaka ya 80 hapakuwa na televisheni nyumbani isipokuwa radio. Hadithi hizo zilikuwa mithili ya tamthlia za leo zilizoanza tangu nyakati za uumbaji, Adamu na Hawa katika bustani ya Eden, historia ya Uyahudi ya kale mpaka maisha ya Bwana Yesu Kristo.

Kila baada ya masimulizi hayo yaliyonukuu vifungu vya biblia, tulijifunza namna gani mambo hayo yalihusianishwa na maisha yetu, tulisisimuka kweli kweli.

Mambo mengi tuliyojifunza nyakati hizo, bado ninayakumbuka mpaka leo. Nikiwa na umri mdogo, nisioweza kuukumbuka kwa uhakika, nilikuwa na uwezo wa kusimulia matukio mengi ya kihistoria katika biblia ingawa sikuwa najua kusoma. Niliweza kukariri mistari mingi ya biblia pasipo kukosea.

Sauti ya mzee haikuondoka kwenye ufahamu wangu. Kila mara katika utoto na ujana wangu ningeweza kumsikia akitusimulia mambo mbalimbali. Hata hivi leo, kuna nyakati ninapofanya maamuzi ya kimaisha, nakumbuka sauti niliyozoea kuisikia zaidi ya miaka 30 iliyopita. Ndani yangu, kuna sauti inayoninong’oneza kunielekeza kipi ni sahihi kufanya na kipi hakifai. Sauti hiyo imekuwa sehemu ya maisha yangu hata leo.

 

Miaka zaidi ya 30 baadae, nami nimekuwa mzazi mwenye watoto wawili. Nimekuwa nikitafakari namna gani nami nimeweza kufanya yale aliyoyafanya baba yangu kwangu zaidi ya miaka 30 iliyopita. Je, nimejenga desturi za kukaa na wanangu kama alivyofanya baba yangu? Je, nimepata muda wa kuwajengea watoto misingi ya kiimani kama alivyofanya mzee wangu?

Suala la imani lina nafasi yake kama sehemu muhimu ya ukuaji wa mtoto. Kama ambavyo mtoto anahitaji kujifunza kuwasiliana na watu wanaomzunguka, anahitaji pia kujenga uelewa wa masuala yanayohusu ulimwengu usioonekana. Wapi tumetoka kama binadamu, tumekuja kufanya nini hapa duniani, na wapi tunakwenda baada ya maisha ya haya, hiyo ndio imani. Bila kuyaelewa mambo haya, ukuaji wa mtoto unakuwa haujakamilika.

Mtoto aliyelelewa vyema kiimani, ana uwezo mzuri zaidi wa kuishi maisha yenye kiasi, yanayoongozwa na misingi fulani, kuliko mtoto aliyekua bila kujifunza misingi imani.

Ilivyo, ni kwamba mzazi ndiye mwalimu wa kwanza kwa mtoto katika maeneo yote ya kimaisha ikiwamo imani. Hakuna mtu mwingine mwenye wajibu wa kuhakikisha mtoto anayaelewa masuala ya msingi yanayohusiana na imani  kama mzazi.

Tusitie bidii katika kuhakikisha watoto wanafaulu masomo yao ya darasani, tukasahau kuhakikisha wamejifunza kile tunachokiamini kama binadamu. Kama ni kweli tusingependa kuona watoto wakiasi kile tunachokiamini, tuna kila sababu kufanya bidii ya kutenga muda wa kuwekeza vyema katika maisha yao ya kiimani. Tunavuna sawa sawa na kile tulichowekeza.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles