ABUJA, NIGERIA
VIKOSI vya Jeshi la Nigeria vimeshindwa kumkamata Kiongozi wa Kundi la Wapiganaji wa Boko Haram, Abubakar Shekau katika operesheni maalum ya kumsaka.
Kwa mujibu wa video ambayo Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) limeiona, wanajeshi wa Nigeria walionekana wakielekea katika kambi ya Shekau kwenye misitu ya Sambisa, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Hata hivyo, baada ya siku nne za kumsaka katika ngome hiyo wanajeshi hao waliamriwa kusitisha safari yao.
Muda mfupi baada ya amri hiyo, askari hao walishambuliwa na wapiganaji waliokuwa na gari lililojaa mabomu.
Katika shambulio hilo, wanajeshi saba wa Nigeria na Cameroon waliuawa.
Hadi vikosi vya Nigeria vinajipanga upya kuwakabili washambuliaji, inadaiwa Shekau alitumia mwanya huo kutoroka.
Serikali ya Nigeria wiki iliyopita ilitangaza zawadi ya Dola za Marekani 8,000 kwa mtu atakayetoa taarifa za kuwezesha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kundi la Boko Haram.
Kundi hilo liliwahi kuteka wanafunzi wasichana zaidi ya 200 wa Chibok, lilifanya tena jaribio la kuwateka wanafunzi na walimu Kaskazini mwa Nigeria.