Na Murugwa Thomas – Tabora
JOPO la majaji wanne kutoka Mahakama ya rufaa wakiongozwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma wanatarajiwa kusikiliza rufani zilizopo Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa wa kanda hiyo, Amir Msumi jopo hilo linatarajia kusikiliza rufani 31 kwa muda wa siku 23.
Msumi aliwataja majaji wengine watakasikiliza rufani hizo kuwa ni pamoja na Sauda Mjasiri, Stella Mugasha na Jaji Shaban Lwila.
Alisema katika muda huo, majaji hao wanatarajia kusikiliza na kutoa uamuzi kwa rufaa 20 zikiwamo rufaa tatu za madai, maombi ya madai saba likiwamo moja la jinai.
“Rufaa 13 ni za muda mrefu ambazo zilikuwapo mahakamani hapa zaidi ya miaka miwili tangu zilipofunguliwa na 18 za muda wa kati,” alisema Msajili huyo.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imeagiza Ofisi ya Masijala ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Magereza kutafuta nyaraka za kumbukumbu za kesi ya Kasaboya Nyabasi ili rufaa yake iliyofunguliwa iweze kusikilizwa mapema.
Agizo hilo limetolewa na jopo la majaji hao ambao walitaka kusikiliza rufaa kesi hiyo ya jinai, namba 173/2015 baada ya kukuta jarada lake halina kumbukumbu muhimu kama nakala za uamuzi wa mahakama za chini.
Wakati huo huo, mahakama hiyo imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi hadi Februari 19, 2018 kwa madai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Kesi hiyo namba 3/2017 2018 inawahusu watumishi watano wa Benki ya Posta mkoani humo pamoja na watu wengine 10.