Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM), umesema wakati huu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikifikisha miaka 41 tangu kuundwa kwake Februari 5, mwaka 1977, vijana wa chama hicho wanapaswa kuheshimu, kutambua na kuthamini mchango wa waasisi waliopitisha wazo la kuunganisha vyama vya TANU na ASP.
Umoja huo umeeleza uamuzi wa viongozi wakuu wa vyama hivyo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi na halmashauri kuu za vyama hivyo unahitaji kuenziwa, kutunzwa na kutambuliwa.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka aliyasema hayo jana, baada ya kumalizika kikao cha kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika Ofisi Kuu ya CCM, Kiswandui mjini Zanzibar.
Alisema kitendo cha kuungana TANU na ASP, kimeleta mafaniko makubwa kisiasa kwa kukifanya chama kipya cha CCM kiwe na nguvu kubwa kisiasa, sera bora, oganaizehsheni ya uhakika, mikakati na kuimarika kwa nidhamu ndani ya chama .
Alisema kimsingi viongozi hao waliona mbali kisiasa kwa kutumia ‘darubini’ kali ya kisiasa na kubaini ikiwa vyama hivyo vitaungana maadui wa ndani na nje watapata pigo.
“Tumefika hapa tulipo, chama chetu kikifikisha miaka 41 kwa kweli ni jambo la kujivunia. Wazee wetu walichemsha bongo na kuona mbali zaidi. CCM imepata uimara licha ya kupigajia maslahi ya wakulima na wafanyakazi,” alisema Shaka.
Alisema chama hicho kimepata mafanikio makubwa kwa kusimamia sera za msingi katika malengo ya kuendeleza amani, kudumisha umoja wa kitaifa, kuleta usawa, kutetea haki za wanyonge na kupigania maslahi ya watu.
“Wananchi wamelitumia soko la uwapo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar chini ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kujijenga kiuchumi. Ustawi wa jamii umekuwa kutokana na utulivu, usalama wa nchi, ulinzi wa maisha ya watu na mali zao. Hakuna ukorofi na utapitapi kwakuwa kinatawala chama makini chenye misingi,” alisisitiza .