29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MSWADA MFUKO HIFADHI YA JAMII WANG’ATA, KUPULIZA

Na Ester Mbussi – Dodoma


SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa mwaka 2017, ambao una takribani mapendekezo 17 yanayouma na kupuliza.

Mapendekezo hayo, ni pamoja na kuunganisha mifuko ya LAPF, PPF, GEPF na PSPF na kuanzisha mfuko mmoja kwa watumishi wa umma na kufuta sheria zilizoanzisha mifuko hiyo.

Mswada huo pia unapendekeza utoaji wa mafao manane ambayo ni fao la pensheni, warithi, ulemavu, uzazi, ukosefu wa ajira, ugonjwa na fao la kufiwa.

Pia unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kuufanya mfuko huo kuwahudumia wafanyakazi sekta binafsi.

Kwa mujibu wa muswada huo uliowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, mswada huo unapendekeza kuanzishwa kwa fao la upotevu wa ajira (Unemployment Benefit), ili kuondoa changamoto ya muda mrefu ya wanachama kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Alisema watakaonufaika na fao hilo ni wanachama ambao hawajafikisha umri wa miaka 55.

“Aidha, mwanachama atakayenufaika na fao hilo pia ni yule ambaye hajaacha kazi kwa matakwa yake, awe Mtanzania, awe amechangia kwa kipindi kisichopungua miezi 18 na ametoa uthibitisho kwa mkurugenzi kuwa hajaweza kupata kazi nyingine.

“Aidha, mfuko utamlipa mwanachama aliyekidhi vigezo mafao yake hata kama mwajiri hajawasilisha michango na baadaye mfuko utafuatilia michango ambayo haijawasilishwa kutoka kwa mwajiri,” alisema.

Kipengele hicho cha fao la upotevu wa ajira, kilizua mjadala baada ya baadhi ya wabunge kudai ni fao la kujitoa limeletwa kivingine.

Mhagama alisema mswada huo pia unapendekeza kuboresha masharti kuhusu fao la uzazi ambapo licha ya kupata fedha taslimu baada ya kujifungua, mwanachama pia atapata huduma ya matibabu kabla na baada ya kujifungua endapo huduma hizo hazilipwi na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Mhagama alisema fao hilo litatolewa mara nne kwa mwanachama katika kipindi chake chote cha ajira.

“Sheria hii inalenga kuimarisha mfumo wa usimamizi na udhibiti wa sekta ili kuwezesha Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii (SRRA) kuendelea kusimamia sekta hiyo ili kuhakikisha mabadiliko hayaathiri kwa namna yoyote masilahi ya wanachama wastaafu,” alisema Mhagama.

Alisema muswada huo ukipita na kuwa sheria, wanachama wa mifuko hiyo watajipatia mikopo ya nyumba na shughuli nyingine za kiuchumi kwa riba nafuu.

Mhagama alisema lengo la kuunganisha mifuko hiyo ni kuondoa uwepo wa mifuko mingi ya pensheni inayotoa mafao yanayofanana na kupunguza gharama za uendeshaji.

Alisema hatua hiyo pia itapunguza gharama za uendeshaji kutoa viwango vya asilimia 19 hadi asilimia tisa iliyowekwa na mdhibiti, kupunguza migogoro baina ya mifuko, kuboresha mafao ya wanachama na kuongeza tija katika sekta ya hifadhi ya jamii.

“Sheria inaweka utaratibu bora na rahisi wa wanachama wa mifuko iliyounganishwa kuhamia kwenye mfuko mpya bila kuathiri mafao yao na uendelevu wa mifuko mipya na wanachama waliopo katika sekta binafsi, ambao kwa sasa wanaochangia kwenye mifuko hawatahamishwa na badala yake utaratibu mpya wa mifuko miwili utaanza kwa wanachama watakaoajiriwa baada ya sheria.

“Pia hiyo imeweka bayana kuwa mafao na michango ya wanachama haitatozwa kodi kama ilivyokwishabainishwa katika sheria za kodi na viwango vya uchangiaji na namna ya uchangiaji katika mfuko, ambapo kiwango cha uchangiaji kitakuwa asilimia 20 huku mwajiri atachangia asilimia 15 na mwajiriwa akichangia asilimia tano ya mshahara,” alisema.

KAMBI RASMI YA UPINZANI

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Msemaji wa Kambi hiyo, Esther Bulaya, alisema wanashauri kuanzishwa kwa mchakato wa kuifuta SSRA kwani kuendelea kuwepo kunaongeza gharama zisizokuwa za lazima.

“Kifungu cha 24 cha muswada kinatoa ruhusa kwa mwanachama kujitoa kwa sharti la kupata kibali cha bodi na kisha bodi kujiridhisha kuwa mwanachama amekidhi matakwa yaliyowekwa.

“Umuhimu wa fao la kujitoa kama sheria ya PPF na PSPF zilizvyokuwa zinahitaji, tukumbuke kuwa kanuni zinaletwa na SSRA kujaribu kuzuia fao la kujitoa ambalo lilileta mtafaruku kwa wanachama, hasa wale waliokuwa wameajiriwa katika sekta ya madini.

“Aidha, vifungu vya 66 na 67 vya muswada vinatoa uhuru kwa Mkurugenzi Mkuu wa PSPF kuomba kibali cha mahakama ili kukamata mali za mwajiri, lakini akashindwa kulipa wakati kifungu cha 72 kinazuia mali za mfuko kukamatwa na kunadiwa bila kuwepo kibali cha waziri, Kambi Rasmi inauliza, kwanini mali zake zisikamatwe kama kutakuwa na amri ya kufanya hivyo, hii tunaona ni ‘double standard’ inayowekwa katika muswada huu,” alisema Bulaya.

 

MAONI YA KAMATI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema kuunganishwa kwa mifuko hiyo kutapunguza gharama za uendeshaji.

Alisema mwaka 2014/15 LAPF pekee ilitumia Sh bilioni 1.8 wakati GEPF ikitumia Sh milioni 300, tofauti ya Sh bilioni 1.5 sawa na asilimia 83.3 kwa gharama za uendeshaji wa bodi ya wadhamini.

Serukamba pia alisema kamati yake inashauri Serikali iongeze aina mbili za mafao kutoka nane yanayotolewa na mfuko hadi 10 kwa kuongeza fao la elimu na fao la mkono wa kwaheri (gratuity benefit).

 

MICHANGO YA WABUNGE

Akichangia maoni kuhusu muswada huo, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele, alisema kutokana na kuondoa fao la matibabu ambalo lilikuwa likitolewa na mifuko mingine, ni vyema Serikali ikaangalia utaratibu wa kuwawezesha watumishi kupata huduma hiyo kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

Alisema Watanzania wengi wako katika sekta isiyo rasmi na wengi hawaratibiwi na mfuko wowote, kwahiyo uamuzi huu unawafanya wengi waratibiwe na utawanufaisha wengi.

“Napendekeza Serikali ilete marekebisho, iongeze fao la bima ya afya ili wanachama watakaochangia katika mfuko mpya utakaoanzishwa katika fao hili waweze kuchangia tena NHIF.

“Mwenyekiti ukitazama kwa makini utaona watumishi wa umma watakuwa wanachangia mara mbili, wanakatwa NHIF ili wachangie huduma, lakini pia wanakatwa huku kwenye mfuko, sasa fedha hizo zielekezwe NHIF kwa wanachama wapya ili kuwaondolea kuchangia mara mbili,” alisema.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alisema mfumo wa nchi unahusisha watu ambao wameajiriwa katika sekta rasmi tu, kwahiyo kuna haja ya kuangalia utekelezaji wa kisera na kisheria katika hifadhi za jamii ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

“Leo hii korosho ina bei nzuri sana na wananchi wamepata fedha nyingi, lakini kesho bei ya soko la dunia ikiporomoka watu watalia kwa sababu hatuna mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wakulima ambao tungeweza kuwapa fao la bei pale ambapo bei zitakuwa zimetetereka.

“Sasa hivi NSSF ina watu 600,000, Serikali inaenda kutunga sheria kuwaondoa watu 600,000 kwenye takwa la kisheria la bima ya afya, naelewa mkanganyiko ambao Serikali inaupata kwamba inataka bima za afya zote ziunganishwe NHIF.

“Inaeleweka tunachopaswa kusema kwamba fao hilo litatolewa na NHIF kwa hiyo NSSF ichukue ile michango ambayo imetolewa na wanachama kwamba asilimia ngapi ya michango inalipia bima ya afya ipelekwe huko na ukiwa na kadi ya NSSF basi moja kwa moja unakuwa mwanachama wa NHIF,” alisema Zitto.

Naye Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), alisema ukokotoaji wa mafao lazima uwekwe kwenye sheria na si uingizwe kwenye kanuni zitakazotungwa na waziri.

Alisema ukokotoaji ukiwekwa wazi kwenye sheria utamwezesha mfanyakazi kufahamu kiwango halisi cha mafao atakachokipata pindi akistaafu.

Pia alisema kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kusiweke kando faida muhimu zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya mifuko hiyo, hususani fao la matibabu na elimu.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. iNAONEKANA Mfuko mpya unakuwa na manufaa makubwa baada ya kuondoa utaratibu wa kukata kodi .Il Kanuni ya Ukokotoaji Mafao iwekwe wazi kwa wadau.
    Ahsante Waziri Jenesia Mhagama kwa kazi nzuri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles