29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MKUU ATOA ONYO KWA VIONGOZI

NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM


JAJI Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, amewataka viongozi wa Serikali kujiepusha kuingilia mamlaka ya kikatiba ya mahakama na kusema atakayefanya hivyo ataitwa kujieleza kwanini asichukuliwe hatua za kisheria kwani wanayo nguvu hiyo.

Profesa Juma alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu maonyesho ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.

Alisema mamlaka moja inapoingia katika mamlaka nyingine, tayari misingi ya katiba inaondoka.
“Nawakumbusha wananchi na viongozi mbalimbali nje ya mahakama, kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, mamlaka ya utoaji haki ni ya mahakama tu.

“Nawasihi viongozi wote wa Serikali wenye mamlaka za kikatiba na kisheria, wabaki ndani ya maeneo yao ya kikatiba na wajiepushe kuingilia maeneo yaliyo ndani ya haki, hadhi na mamlaka ya kikatiba ya mahakama.

“Ibara ya 107A (1) ya katiba inazungumzia mamlaka ya utoaji haki, inatukumbusha kwamba mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar na kwahiyo, hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.

“Sheria ndiyo inatakiwa kupewa nguvu kwa sababu nguvu ya Serikali ni sheria, siyo mtu, ni sheria, sheria ikipewa nguvu unaitumia, ikikupa mamlaka unaitumia.
“Siasa haikupi nguvu, sheria ndiyo inakupa nguvu, tujaribu kubaki ndani ya sheria, ndani ya katiba, hakutakuwa na migongano,” alisema Jaji Mkuu.

Alisema nguvu na mamlaka aliyopewa mtu mwingine mahakama haiwezi kuingilia, kama mamlaka ambayo amepewa polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, jaji au hakimu hawezi kumwingilia.

“Vilevile tunawataka wale ambao wamepewa mamlaka yao wabaki huko waliko na tukifanya hivyo hatutakuwa na migongano yoyote kama tutabaki kwenye maeneo yetu.
“Tutakuwa wakali sana kuanzia sasa katika nafasi ya mahakimu, majaji tutakuwa wakali watu wakiingia kwenye anga zetu.

“Msingi wa kuwakumbusha wenye mamlaka nadhani ni kwamba mambo yanatakiwa kuwa kwa mujibu wa katiba ambapo kazi moja ya katiba ni kuzigawa mamlaka,” alisema.

Profesa Juma alisema mamlaka moja inapoingia katika mamlaka nyingine, tayari unaondoka katika misingi ya Katiba.
“Chanzo changu cha kutoa wito huu ni kutoka kwenu waandishi wa habari, mmekuwa mkitoa taarifa amri za mahakama zinadharauliwa, zinavunjwa.

“Sasa nyie kama watu wa kutoa taarifa mmezikusanya na kuniletea, nimeona vizuri nichukue muda huu kuwaambia hasa mahakimu, kuwakumbusha kwamba anayelinda haki na uhuru wa mahakama ni hakimu na jaji na wanaohusika.

“Kama unatoa amri unaona kuna mtu anaivunja, kuna ule utaratibu wetu wa kumwita yule mtu na kumuuliza kwanini asichukuliwe hatua na kuna kesi nyingi sana za Mahakama Kuu na Rufani ambazo zimetoa maelezo hayo.
“Mimi nawaomba mahakimu ambao kwa bahati mbaya amri zao zinavunjwa na hawaonekani wakichukua hatua, nadhani imefika wakati tuwe kama Bunge wanavyofanya, ukiingia katika anga za Bunge utaitwa mbele ya kamati, utaulizwa maswali na hatua zote zitachukuliwa.

“Mahakama tuna nguvu kama hiyo na siyo Jaji Mkuu tu mwenye nguvu kama hizo, nguvu zipo kwenye kila mahakama za mwanzo, wilaya na hakimu mkazi, asitokee mtu akajivika kofia ya mahakama, atachukuliwa hatua,” alisema.

Akizungumzia Siku ya Sheria, alisema watatumia siku tano kuanzia Januari 27 hadi 31, kutoa elimu ya sheria kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo.
Alisema utoaji wa elimu ya sheria na msaada wa kisheria utaanza rasmi Januari 27 katika Viwanja vya Mnazi mmoja na kufikia tamati Februari mosi.

Maonyesho hayo yatatanguliwa na matembezi maalumu ya kuadhimisha wiki hiyo yatakayofanyika Januari 28 yakiongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wiki hiyo pia itatumika kuzindua majengo ya mahakama, ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Kawe, Kituo cha Kisasa cha Mafunzo Kisutu, Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mahakama ya Wilaya Mkuranga na Mahakama ya Wilaya Kigamboni.

“Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kitafanyika Februari mosi mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Rais Dk. John Magufuli ambapo maudhui kwa mwaka huu ni ‘Matumizi ya Tehama katika utoaji haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili’,” alisema Profesa Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles