Panya waharibifu wamevamia mashamba ya mahindi ya wananchi wilayani Handeni, mkoani Tanga na kula mahindi yote hatua inayodaiwa kuleta hofu ya kukumbwa na baa la njaa.
Wakizungumza na Mtanzania Digital baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kwediwawala wilayani humo, wamesema panya hao wamevamia mashamba zaidi ya hekari 30 za mahindi yaliyokuwa yamekomaa ambayo walilima katika kipindi cha mvua za vuli.
Wamesema panya wamewasababishia hasara kubwa kwani hakuna walichobakiza mashambani humo na kwa sasa wameanza kuingia majumbani mwetu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho, amesema tayari malalamiko yao wameshayafikisha Ofisi ya Kilimo ya Wilaya ya Handeni.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema ofisi yake ina taarifa za kuwepo kwa panya hao waharibifu na kwamba tayari wamekwishachukua hatua ya kupeleka barua wizara ya kilimo ili kuomba dawa ya kuwateketeza.
“Niwatoe hofu wananchi na pia nawaomba wawe na subirakwani serikali inatambua uwepo wa tatizo hilo na itahakikisha wadudu hao hawatakuwapo katika msimu ujao wa kilimo,” amesema Gondwe.