24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

JAMES MCCARTHY AVUNJIKA MGUU MARA MBILI

LONDON, ENGLAND


KLABU ya Everton imepata majanga mapya, baada ya juzi kiungo wao, James McCarthy, kuvunjika mguu mara mbili katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya West Brom, huku mchezo huo ukimalizika kwa sare ya 1-1.

Tukio hilo la kuvunjika mguu lilitokea baada ya kuchezewa vibaya na nyota wa West Brom, Salomon Rondon ambaye alikuwa na lengo la kuupiga mpira na hatimaye kuupiga mguu wa mchezaji huyo na kuvunjika mara mbili.

Katika mchezo huo, West Brom walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika za awali kwenye Uwanja wa Goodison Park na kuwanyamazisha mashabiki wa uwanja huo baada ya bao la Jay Rodriguez, lakini baadaye wenyeji Everton waliweza kusawazisha.

Kocha wa klabu hiyo ya Everton, Sam Allardyce, amethibitisha huku akisema kwamba wamepata pigo kubwa kuumia kwa mchezaji huyo.

“Ni pigo kubwa sana kwa klabu ya Everton kutokana na mchezaji wetu James McCarthy kuvunjika mguu, tunaamini mchezaji huyo atarudi uwanjani muda mfupi mara baada ya kupona, lakini kwa sasa ametuacha kwenye wakati mgumu.

“Lilikuwa ni tukio la bahati mbaya na mara nyingi linatokea kwenye maisha ya soka, hivyo tunatakiwa kuendelea kumpa sapoti na kumfariji ili aweze kuondoa wasiwasi,” alisema Allardyce.

Baada ya mchezaji huyo kuumia na kutolewa nje, nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji wao, Wayne Rooney, katika dakika ya 57, lakini bado la Everton liliwekwa wavuni na mshambuliaji wao, Oumar Niasse katika dakika ya 70, huku pasi ya mwisho ikitoka kwa mshambuliaji wao mpya Theo Walcott.

Hata hivyo, Rondon ambaye amemvunja mguu McCarthy, alikuwa hana furaha baada ya tukio hilo huku akiamini kuwa amempotezea malengo yake mchezaji huyo katika kipindi hiki cha michuano ya Ligi Kuu.

“Nimejisikia vibaya sana kwa kile kilichotokea, ilikuwa bahati mbaya na ninaamini atarudi kwenye hali yake muda mfupi na ninamuombea aweze kurudi katika hali yake ya zamani ili kuitumikia klabu yake kama kawaida,” alisema Rondon.

Mchezaji huyo alijikuta akitokwa na machozi, huku akizungukwa na wachezaji wenzake kutokana na tukio alilolifanya.

McCarthy amekuwa katika kikosi cha Everton tangu mwaka 2013, akitokea klabu ya Wigan Athletic kwa kitita cha pauni milioni 13, lakini msimu huu amecheza jumla ya michezo minne ya Ligi Kuu kutokana na kusumbuliwa na tatizo la goti na nyama za paja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles