25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

RONALDINHO ANASTAAFU HUKU MASHABIKI WAKIMUHITAJI  

NA BADI MCHOMOLO


RONALDO de Assis Moreira, ana majina mengi, lakini maarufu anajulikana kwa jina la Ronaldinho Gaucho, fundi mpira ambeya hajadumu sana kwenye ulimwengu wa soka, ila jina lake litaendelea kudumu hadi mwisho wa maisha yake.

Ronaldinho alitokea kwenye familia ya watoto watatu wakike akiwa mmoja, lakini Ronaldinho alikuwa wa mwisho kuzaliwa katika familia ya mzee Joao de Assis Moreira, ambaye alikuwa anafanya kazi kwenye meli. Alizaliwa Machi 21, 1980.

Maisha ya familia hiyo kwenye mji wa Porto Alegre huko nchini Brazili yalikuwa ya kawaida sana kwa kuwa baba yao alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo, lakini maisha yao yalianza kubadilika baada ya kaka wa mchezaji huyo Roberto de Assis kusajiliwa na klabu ya Gremia.

Ronaldinho alianza kupenda mpira huku akiwa na umri wa miaka nane, alipata nafasi ya kucheza timu za mtaani na alionesha kiwango cha hali ya juu, alipata sifa nyingi kwa kuwa alionekana mchezaji mfupi na mdogo kwenye michuano ya mtaani, lakini alikuwa na uwezo wa pekee.

Alianza kutambulika akiwa na umri wa miaka 13 baada ya vyombo vya habari kumuandika na kumuita jina la Ronaldinho kutokana na kupachika mabao 23 peke yake kwenye mchezo mmoja wa ligi za mtaani, huku timu yake ikishinda mabao 23-0.

Kutokana na kiwango hicho, Ronaldinho akachukuliwa na timu ya vijana ya Gremio ambayo kaka yake alikuwa anacheza ya wakubwa, hivyo mwaka 1998 alipandishwa timu kubwa na kuonesha uwezo wake hadi 2001 alipojiunga na PSG.

Dunia ilianza kumtambua vizuri mchezaji huyo mwaka 2003 alipojiunga na klabu ya Barcelona hadi pale alipoondoka mwaka 2008 na kujiunga na klabu ya AC Milan.

Miaka mitano akiwa na klabu ya Barcelona aliweza kuitikisa dunia kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira uwanjani, kukimbia na mpira, uwezo wa kuuchezea mpira, kufunga mabao, kutengeneza nafasi, hivyo alitajwa kuwa ni mchezaji mwenye uwezo wa pekee duniani.

Dunia ilitambani kumuona mchezaji huyo zaidi ya miaka 10 akiwa na kiwango ambacho alikionesha katika klabu ya Barcelona, lakini kitu kinachopendwa zaidi na watu wengi hakiwezi kudumu sana, ndivyo kilichotokea kwa Ronaldinho.

Mchezaji huyo aliwahi kushangaza dunia baada ya kupigiwa makofi na mashabiki wa Real Madrid kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu huku akiwa na klabu yake ya Barcelona, hiyo ni kutokana na na kukubalika na mashabiki duniani.

Alipendwa na kila mtu, wengi walitamani kumuona mchezaji huyo akiendelea kuwa kuwa kijana ili atoe burudani ya soka viwanjani, lakini hakuna marefu yasio na mwisho, wiki iliopita mchezaji huyo ametangaza kustaafu soka rasmi.

Tangu alipoondoka Barcelona, soka lake lilianza kushuka, lakini aliendelea kupata nafasi ya kucheza timu mbalimbali kama vile Flamengo, Atletico Mineiro, Queretaro na mara ya mwisho alijiunga na klabu ya Fluminense hadi 2015.

Hapo ndipo soka lake la kulipwa lilifikia mwisho mwaka 2015, lakini aliendelea kucheza soka kwenye mabonanza mbalimbali kwa ajili ya kuchangia mifuko ya kijamii. Kitendo hicho kilimfanya mchezaji huyo aendelee kuwa mfalme kwa mashabiki wake kwa kuwa bado aliendelea kuonesha vitu ambavyo mastaa wengine walishindwa kuvifanya.

Wapo mashabiki ambao walikuwa wanatamani kumuona mchezaji huyo akirudi kwenye muchuano mbalimbali hasa ile ya Ligi Kuu, kwa kuwa vile ambavyo alikuwa anavifanya kwenye mabonanza havipatikani hata kwenye Ligi hizo, lakini ndio basi tena, kilichobaki ni kusubiri mchezaji huyo akiwaaga mashabiki wake kwa namna yake.

Kaka wa mchezaji huyo Roberto de Assis Moreira, ambaye alikuwa wakala wake, ametangaza kuwa wanatarajia kuandaa tukio la kuwaaga mashabiki wake nchini Brazil, barani Ulaya na Asia, hivyo klabu ya Barcelona na kampuni ya Nike itahusika kusimamia suala hilo mara baada ya kumalizika kwa Kombe la dunia mwaka huu nchini Urusi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles