- Ni yule aliyeipa Cameroon ubingwa wa Afrika
Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
HATIMAYE klabu ya Simba imemtambulisha rasmi kocha wa zamani timu ya Taifa ya Cameroon Mfaransa, Pierre Lechantre, kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho.
Lechantre ambaye aliiongoza Cameroon kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mwaka 2000, anakuja kuchukua nafasi ya Joseph Omog, aliyetemwa baada ya timu hiyo kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam.
Mfaransa huyo aliiongoza Cameroon kutwaa ubingwa huo baada ya kuichapa Nigeria kwa mikwaju ya penalti 4-3, katika mchezo wa fainali uliochezwa Februari 13 kwenye Uwanja wa Taifa Lagos, nchini Nigeria.
Mchezo huo ulifika hatua ya penalti baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 kwa kufungana mabao 2-2.
Katika mchezo huo, Cameroon iliwakilishwa na wachezaji mahiri kama Samuel Eto’o, Partick Mboma na Marc Vivian Foe ambaye kwa sasa ni marehemu, huku Nigeria ikiwa na Celestine Babayaro, Taribo West na Jay Jay Okocha.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 67, alichukua jukumu la kuinoa Cameroon kuanzia mwaka 1999 hadi 2001 alipotimkia Qatar.
Lechantre ambaye pia ni mshambuliaji wa zamani wa timu za FC Monaco na Olimpic Marseille za Ufaransa, amewahi kutwaa tuzo mbili ya kocha bora Afrika 2001, pia kocha bora Asia mwaka 2012.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara, ilisema kocha huyo ataanza kazi mara moja.
“Simba inayo furaha kubwa kuwajulisha wanachama na mashabiki wake kwamba, imempata kocha wake mkuu mpya, Mfaransa, Pierre Lechantre, kocha huyu ataanza kazi mara moja akisaidiwa na Masoud Djuma, aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo.
“Lechantre ameambatana na msaidizi wake, Mohammed Aymen Hbib, raia wa Morocco ambaye ni kocha wa viungo,” alisema Manara.
Wasifu kamili
KLABU ALIZOCHEZEA
1970-1975 Sochaux
1975-1976 Monac
1976-1979 Laval
1979-1980 Lens
1980-1981 Marseille
1981-1983 Reims
1983-1986 Red Star
1986-1989 Paris FC
TIMU ALIZOFUNDISHA
1987-1992 Paris FC
1992-1995 Le Perreux
1999-2001 Cameroon
2002-2003 Qatar
2003 Al-Ahli
2003-2004 Al-Siliya
2005-2006 Mali
2006-2007 Al Rayyan
2007-2008 MAS Fes
2009-2010 Club Africain
2010 CS Sfaxien
2012 AL Arabi
2014-2015 AL-Lttihad Club Tripoli
2016 Congo