29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

BENDERA YA TANZANIA YAZIPONZA MELI MBILI

Na TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

SERIKALI imetangaza kuzifutia usajili meli mbili zilizokamatwa zikisafirisha dawa za kulevya na silaha huku zikipeperusha bendera ya Tanzania.

Desemba 27, mwaka jana meli inayojulikana kwa jina la Kaluba yenye namba za usajili IMO 6828753 ilikamatwa Jamhuri ya Dominica ikiwa imebeba Kilo 1,600 za dawa za kulevya .

Sambamba na hiyo, Januari 11, mwaka huu meli iitwayo Andromeda yenye namba za usajili 7614666 ilikamatwa nchini Ugiriki ikiwa imebeba vilipuzi kinyume na sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema meli hizo zinatakiwa kuishusha bendera ya Tanzania.

“Tumefuta usajili wa meli hizo na kuwataka washushe bendera yetu na wapambane na tatizo hilo wenyewe na sisi tutatoa ushirikiano utakapohitajika,” alisema Samia.

Alisema meli zote mbili zimesajiliwa Tanzania kupitia taasisi ya  Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusajili meli za nje.

“Tanzania imejidhatiti na imedhamiria kutekeleza majukumu yake yaliyoelezwa katika  mikataba ya kimataifa, ikiwamo kushirikiana na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa katika kupiga vita usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha,” alisema Samia.

Alisema serikali imeona haja ya kuunda kamati ya pamoja ya wataalamu kutoka bara na visiwani itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kupitia upya usajili uliokwisha fanyika na kuzihakiki taarifa za meli zilizosajiliwa nchini.

“Tutafanya mapitio ya sheria zetu kuzipa nguvu taasisi zinazosimamia usajili wa meli huku timu ya wataalamu itaangalia kwa  makini kodi zinazotozwa na mchango wake ili tusiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili,” alisema Samia.

Aliongeza kuwa  wataendelea kuzipa ruhusa nchi  nyingine kukamata na kuzipekua meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania wakati wowote zinapohisiwa kuwa zinafanya uhalifu, au masuala ambayo haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazokubalika kimataifa.

Wakati huo huo, Samia amevitaka viwanda vinavyojengwa nchini kusafisha na kuyatibu maji kabla ya kuyatiririsha katika mitaro ili kulinda na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza katika ziara aliyoifanya manispaa za Ilala na Temeke, Samia alisema viwanda hivyo vihakikishe vinatunza mazingira kwa kutiririsha maji yaliyotibiwa .

“Nimepata taarifa kuwa kuna viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa na watu kutoka China, naamini watatumia mitaro hii kutiririsha maji ya viwandani lakini niwaombe wayatibu kwanza ndipo waingize katika mitaro yetu,” alisema Samia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles