Jalada la kesi ya aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya kumiliki mali nyingi zisizo na maelezo, kughushi na kutakatisha fedha limerudishwa Takukuru kwa upelelezi zaidi.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon amedai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa leo Alhamisi Januari 18.
Wankyo amedai jalada la kesi hiyo litarejeshwa tena kwa DPP ili kujiridhisha kama maelekezo aliyotoa yametekelezwa.
Naye Wakili wa utetezi, Alex Mushumbusi amedai hategemei kuona upelelezi unachukua muda mrefu kwa sababu mshtakiwa Gugai alikuwa mtumishi wa taasisi hiyo. Baada ya kusema hayo Hakimu Simba aliahirisha kesi hadi Januari 31, mwaka huu kwa kutajwa.