Na MWANDISHI WETU -MOROGORO
ANNA Mayunga ambaye ni mama mzazi wa wakili maarufu, Peter Kibatala amefariki duniani baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba yake.
Akiongea na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Wakili Kibatala alisema mama yake alifikwa na umauti wakati akikagua eneo la nyumba yake iliyoko eneo Fokoland, SUA mjini Morogoro.
“Baada ya mvua ilinyesha leo (jana) asubuhi saa mbili aliamua kukagua nyumba kwa kuizunguka ili kuona kama maeneo yetu yamepata madhara, ghalfla ukuta wa nyumba ulianguka na kupoteza uhai wa mama,” alisema Kibatala kwa ufupi
Taarifa zaidi zilizopatikana kutoka Morogoro zilieleza kuwa mvua hizo zilibomoa nyumba kadhaa huku nyingine zikizingirwa na maji katika maeneo ya Kata ya Mafisa na Kihonda zilizo katika Manispaa ya Morogoro.
Ilielezwa kuwa mvua hizo zilisababisha adha ikiwamo kuziba njia kadhaa mkoani humo pamoja na mafuriko na hivyo baadhi ya wanafunzi walishindwa kwenda shule.
Baadhi ya wakazi maeneo mbalimbali ya mkoani humo walieleza kuwa mafuriko hayo yaliyakumba zaidi maeneo ya Kichangani, Mazimbu, Chamwino, Mbuyuni, Kilakala, Boma na sabasaba.
“Mvua imesababisha shughuli za biashara na hasa maduka katikati ya Manispaa kufungwa baada ya maji kuingia ndani na kusababisha uharibifu wa bidhaa mbalimbali.
“Madhara mengine ni kuharibika kwa miundombinu ya barabara baada ya kujaa maji. Wananchi walilazimika kuvushwa kwa kubebwa mgongoni kwa Sh1,000
Diwani wa Kata ya Mafisa, Daud Salumu (CCM), alisema nyumba mbili zilizo kwenye kata yake zimebomoka na nyingine zimezingirwa na maji.
Alisema kila mwaka kata yake inakumbwa na mafuriko hivyo ipo haja kwa halmashauri kuangalia namna ya kuepuka mafuriko hayo.
Akizungumzia hali hiyo, Mhandisi wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura), Mkoa wa Morogoro, Lusingi Mashashi alisema wanashirikiana na halmashauri ya manispaa ya Morogoro kuhakikisha miundombinu yote ya barabara inarekebishwa kwa wakati.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Inspekta Shomary Sala alisema eneo la Kihonda polisi walimuokoa mwanafunzi aliyekuwa amesombwa na maji wakati akivuka mto.