MANCHESTER, ENGLAND
BAADA ya klabu ya Tottenham kukubali kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya vinara wa Ligi Kuu England, Man City, kocha wa timu hiyo, Mauricio Pochettino, ameweka wazi kuwa hakuna wa kuuzima moto wa wapinzani hao.
Hata hivyo, kocha huyo amewatupia lawama wachezaji wake kwa kuruhusu bao la mapema katika dakika ya 14 lililowekwa wavuni na kiungo wao, Ilkay Gundogan, mabao mengine yaliwekwa wavuni na Kevin de Bruyne na Raheem Sterling, aliyefunga mabao mawili.
Ushindi huo wa Manchester City unawafanya Tottenham kuwa nyuma dhidi ya vinara hao kwa pointi 21, hivyo kocha huyo anaamini ni kazi kubwa kukipunguza kasi kikosi cha Pep Guardiola.
“Naweza kusema Manchester City wameamua kuonesha kwanini wao ni timu bora kwenye michuano hii ya Ligi Kuu, kwa upande wetu ni wazi tulicheza chini ya kiwango, hali hiyo ilichangia kuwapa wapinzani nafasi ya kutufunga bao la mapema.
“Hatuna la kusema, lakini ukweli ni kwamba Manchester City walistahili kushinda mchezo huo kutokana na ubora wao wa kikosi pamoja na kocha, hakuna timu ambayo inaweza kuzuia kasi yao, lakini chochote kinaweza kutokea kutokana na kuwa soka ni mchezo wa makosa.
“Kwa sasa tunatakiwa kutulia na kuangalia mchezo unaofuata ili kuweza kushinda na kujiweka kwenye nafasi nzuri, ushindani ni mkubwa kwenye michuano hii lakini bado muda upo na tunaamini tutafanya vizuri,” alisema kocha huyo.
Baada ya ushindi huo baadhi ya wachezaji wa timu ya Man City, walionekana kwenye chumba cha kubadilishia nguo na huku wakiwaimba Manchester United badala ya Tottenham, wachezaji hao walirekodi video huku wakiimba ‘Paki basi, paki basi’, wimbo huo moja kwa moja walikuwa wanawaimbia wapinzani hao ambao waliwapa kichapo cha mabao 2-1 wiki moja iliyopita.
Kwa sasa Manchester City wanaongoza kwenye msimamo wa ligi wakiwa na jumla ya pointi 52 baada ya kucheza michezo 18, huku nafasi ya pili ikishikwa na wapinzani wao Manchester United wakiwa na pointi 38 kabla ya mchezo wa jana.