Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amewataka Watanzania kuacha kupambana na umasikini badala yake wajenge ustawi katika shughuli za uzalishaji mali ili kukuza uchumi.
Akiwa katika hafla ya kuadhimisha miaka 25 ya taasisi ya Tanzania Growth Trust (TGT) ambayo awali ilijulikana kama Tanzania Gatsby Trust, katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam, Mwijage alisema kwa muda wa miaka 56, Tanzania imepambana na umasikini lakini hakuna tija inayoonekana.
“Unataka kupambana na umasikini utauweza? Mimi siamini katika changamoto bali nataka wajasiriamali wapate elimu kuhusiana na sekta hii muhimu itakayotusaidia kufikia azma ya uchumi wa viwanda,” alisema.
Alibainisha kuwa kwa sasa wananchi wageukie kujenga uchumi wa viwanda ili kupata ajira na kuzalisha bidhaa zenye viwango kwa soko la ndani na kimataifa, aliwataka wajasiriamali waliohudhuria hafla hiyo kuhakikisha wanapata elimu au taarifa kuhusiana na shughuli wanayotaka kuanzisha.
“Kuna kitu lazima nikiseme kuhusiana na ujasiriamali, kwanini ujenge nyumba halafu uweke wapangaji. Sikatazi mtu kujenga nyumba ya kuishi lakini hapa kuna watu wana nyumba tatu moja anaishi na familia na nyingine mbili amepangisha.
“Hapana nyumba hizi badala ya kupangisha tengeneza kiwanda kidogo cha kuchakata chakula utapata faida,” alisema Mwijage.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa TGT, Oliver Luena, alisema lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ni kuwainua wajasiriamali wadogo kutambua fursa zilizopo katika ardhi ya Tanzania ili waendeshe shughuli zao kwa weledi.
“TGT ilianzishwa baada ya kutambua kwamba, uwezo wa sekta ya viwanda vidogo na vya kati haujatumika kikamilifu kufikia hatua ya kuwawezesha wajasiriamali, wakulima na wananchi kwa ujumla kuondokana na hali ya umasikini, kukosa ajira na vipato duni,” alisema Luena.
Alisema kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (Unido), wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo waliopata elimu juu ya usindikaji.
“Mbali ya mafunzo ya usindikaji lakini pia tulipata fursa ya kushiriki maonyesho mbalimbali ya kimataifa katika bidhaa za aina tofauti zilizotengenezwa na wajasiriamali wadogo katika vikundi, vile vile tumekuwa na biashara ya miche ambayo kwa sasa imeshamiri na ni sehemu ya kujiingizia kipato,” alisema.
Miongoni mwa wanufaika wa taasisi hiyo kutoka Zanzibar aliyewakilisha kikundi cha Fahari, Athumani Kombo, alisema kabla ya kujiunga na TGT walikuwa wakifanya shughuli zao kienyeji, lakini miaka sita iliyopita walitembelewa na maofisa wa taasisi hiyo waliowapa mafunzo na sasa wanafanya kazi zao kwa faida.
“Kikundi chetu kilipotembelewa na maofisa wa TGT miaka sita iliyopita kwanza walionyesha kutoridhishwa, lakini wakatuletea mwalimu kutoka Uingereza akakaa na sisi kwa miaka minne kutuelekeza namna ya kufanya shughuli za uzalishaji mali,” alisema Kombo.