NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amesema majeraha yaliyotokana na risasi zilizoingia mwilini mwake yamepona, isipokuwa viungo.
Pia amesema siku aliyofikishwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, mwili wake ulikuwa vipande vipande baada ya risasi 16 kuingia mwilini.
Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka huu akiwa nje ya nyumba yake mjini Dodoma, alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa na Redio ya Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW).
Katika mahojiano hayo, Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), alisema siku aliyopigwa risasi, kila kiungo cha mwili wake kilikuwa kimechanika.
“Naendelea vizuri, bado sijapona ndiyo maana niko hapa kitandani, ninaposema naendelea vizuri ni kwa sababu majeraha ya risasi yamepona na kwa maelezo ya madaktari, kuna risasi 16 ziliingia katika sehemu mbalimbali za mwili wangu.
“Miezi mitatu ya baada ya lile shambulio la kigaidi, majeraha yamepona, iliyobaki ni kunifanya nitembee na kufanya shughuli zangu kama binadamu wengine. Ni safari ndefu kidogo, lakini hali yangu itarejea kama kawaida.
“Nilifikishwa hapa nikiwa vipande vipande, miguu imevunjika, mikono imevunjika na matumbo yakiwa yamechanwa chanwa, nilikuwa na hali mbaya sana, sikuwa mtu wa kuishi,” alisema Lissu.
Alisema kwa sasa anaendelea vizuri ingawa ni vigumu kurudia hali yake ya awali.
“Kwa mujibu wa madaktari wanaonitibu, wanasema ni safari ndefu kurudi katika hali yangu, lakini nitarejea na kuendelea na shughuli zangu za kawaida,” alisema.
Lissu alisema kuwa mara baada ya kushambuliwa, hakuna kiongozi yeyote wa Bunge aliyefika hospitalini hapo kumjulia hali.
“Ni mwezi wa tatu sasa Spika hajaja, Naibu wake hajaja, Katibu wala kamati inayoshughulikia hawajaja wala kunisaidia kwa namna yoyote,” alisema Lissu.
Alisema msaada huo si fadhila bali ni sheria waliyojiwekea bungeni, kuwa mbunge anapougua na kulazwa ndani au nje ya nchi, anapaswa alipwe gharama zote na Bunge.
“Hakuna sehemu ilipoandikwa ndani ya sheria za uendeshaji wa Bunge kuwa gharama hizo zitalipwa kama mbunge akitibiwa Muhimbili ama India,” alisema.
Akizungumzia kuhusu kauli ya IGP Simon Sirro kuwa alitoa taarifa kwa vyombo vya habari na si kwa jeshi hilo, Lissu alisema jeshi hilo lina namna nyingi za kupata taarifa.
Alisema maisha yake yote atayatumia katika kudai haki kwani anayedai haki ni mpenzi wa Mwenyezi Mungu.
“Nasubiri nipone kama ambavyo madaktari wamesema nitasimama, nitatembea na nitaendelea kudai haki kwa kuwa maandiko yanasema haki huinua taifa,” alisema Lissu.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha CHAUMMA, Hashim Rungwe, alimtembelea na kumjulia hali mwanasheria huyo Mkuu wa Chadema hospitalini jijini Nairobi anakotibiwa.
Mwanasiasa huyo alitoa wito kwa Watanzania kuwa na moyo wa upendo, huku akilaani waliomfanyia kitendo hicho.
Pia alilitaka Jeshi la Polisi na vyombo vya dola kufanya kila njia ili kuwapata watu waliohusika na shambulio dhidi ya Lissu.