MOSCOW, Urusi
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin anatarajia kukutana na wanahabari mahiri wa kimataifa katika mkutano wake wa kila mwaka na vyombo vya habari Alhamisi wiki hii.
Mkutano huo utakaofanyika Alhamisi wiki hii utamkutanisha na wanahabari 1,640 kutoka mataifa mbalimbali kama vile Marekani, Ujerumani, Japan, Ufaransa, China, Poland, Estonia, Urusi na kwingineko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hapa juzi na msemaji wa Ikulu, miongoni mwa wanahabari hao ni Ksenia Sobchak wa Kituo cha televisheni cha Dozhd, ambaye anajiandaa kupambana na Putin katika uchaguzi wa rais wa Urusi.
Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Sobchak kuhudhuria mkutano huo wa Rais Putin baada ya kufanya hivyo mwaka 2014 na 2015.
Mbali na mwandishi huyo mwingine aliyetajwa ni mtangazaji wa kituo cha Redio Ekho Moskvy, Tatiana Shadrina, ambaye Oktoba mwaka huu alishambuliwa na raia kutoka Israeli.
Rais Putin alilaani vikali tukio hilo na kusema kuwa hana cha kulizungumzia zaidi kutokana uhuru wa kujieleza uliopo nchini hapa.
Mkutano huo wa kila mwaka wa Rais Putin na wanahabari unazidi kupata umaarufu, ukiongezeka kwa mahudhurio kutoka waandishi 500 mwaka 2001, hadi idadi ya sasa.