Na JANETH MUSHI-ARUSHA
MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari(Chadema), amemzika kwa heshima mbwa wake, kwa kuokoa maisha yake.
Wakati akimzika mbwa huyo, Nassari alikumbuka ajali ya helkopta aliyoipata mwaka 2015 ambayo alidai bila helkopta hiyo kuangukia kwenye mti asingekuwa hai leo hii.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mbunge huyo alisema kwa kushirikiana na wananchi wa jimbo lake na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, walimzika mbwa huyo juzi Desemba 2 saa 10 jioni.
Waliohudhuria ni Godbles Lema na Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambao wote walishiriki katika mazishi ya mbwa huyo aliyezikwa katika shamba la karibu na nyumbani kwa mbunge huyo.
Katika mazishi ya mbwa huyo ambaye alizikwa kwa heshima ikiwamo kuchimbiwa kaburi ambalo lilizungukwa na watu mbalimbali na kufukiwa kwa utaratibu mithili ya binadamu.
Mbwa huyo alikufa usiku wa kuamkia Desemba 2, nyumbani kwa mbunge huyo katika Kijiji cha Nkwanenkori wilayani Arumeru, baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana ambao walimwua mbwa huyo kwa risasi.
Alisema aliamua kumzika mbwa huyo kwa heshima kwa sababu risasi zilizomwua pengine zingeingia katika mwili wake na kumsababishia kifo.
“Nimeimarika niko sawa namshukuru Mungu niko hao napumua hilo ndiyo kubwa kuliko yote…tulishauriana tumzike vizuri kwa heshima zote kwa sababu kwa kweli alipambana ndiyo maana akauawa na kama asingeuawa yeye ninegweza kuuawa mimi.
“Naamini amechukua risasi ambazo pengine zingeingia kwenye mwili wangu, ni kama mjeshi ambaye amefia vitani akimpigania bosi wake kwa sababu baada ya kusikia milio ya risasi nje ilinichukua muda mrefu kutafuta silaha yangu hadi kutoka nje.
“Tumemzika kwa majonzi kwa sababu amekufa akilinda maisha yangu, hakustahili kifo hicho ila naamini Mungu anaweza kumsaidia mtu kwa kutumia kitu chochote.
“Mwaka 2015 nilinusurika kufa katika ajali ya helkopta na naamini mti ule ndiyo ulisaidia helkopta yetu haikulipuka,” alisema Nassari.
Mbunge huyo alidai kuwa miongoni mwa viongozi waliompigia simu ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ambaye mbali na kumpa pole alimshauri kujiongezea ulinzi.
“Namshukuru Nchemba (Waziri wa Mambo ya Ndani) kwa vile amenipigia simu akanisisitiza niongeze ulinzi, nijiiamrishie ulinzi ili nihakikishe niko salama.
“Akaniambia niongeze gharama binafsi kwa ajili ya usalama wangu kwa sababu mwisho wa yote maisha yangu ni muhimu,” alisema.
Watu wasiojulikana wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Nassari juzi Saa 5:30 usiku ukiwa ni muda mfupi tangu arejee nyumbani kwake akitokea kwenye kongamano la vijana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Julai 2015 mbunge huyo alinusurika kifa baada ya kupata ajali ya helikopta aliyokuwa akiitumia katika harakati za kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Leguruki wilayani Arumeru.
Chanzo cha ajali hiyo kilidaiwa ni helikopta hiyo kupoteza mwelekeo na kumshinda rubani aliyeamua kuishusha na kunasa juu ya mti.