JUMLA ya silaha 136 kutoka kwa wananchi zilikamatwa wakati wa Operesheni Tokomeza.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima, wakati akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati (CCM).
Katika swali lake, Chiligati alitaka kujua idadi ya silaha zilizokamatwa wakati wa operesheni hiyo na lini wamiliki halali wa silaha hizo watarudishiwa silaha zao.
Silima alisema silaha zilizopatikana na kuhifadhiwa katika vituo vya polisi wakati wa zoezi hilo ni pamoja na shotgun 16, bastola moja, riffle 16 na magobore 114.
“Uchunguzi wa awali ulionesha kuwa kati ya silaha 136 zilizokamatwa, ni silaha 16 tu, yaani riffle 4 na shotgun 12 ndizo zinamilikiwa kihalali, silaha zilizobaki zinaendelea kufanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi kuhusiana na matukio mbalimbali ya kiuhalifu,” alisema.
Silima alisema kuhusu zoezi la kuwarejeshea wamiliki silaha zao, itategemea matokeo ya kesi zilizopo mahakamani na uhakiki unaofanywa na polisi utakapokamilika.