Na Christian Bwaya
MAMA Rahma anarudi nyumbani jioni. Rahma anaposikia mlio wa gari ya mama yake, anatoka nje kwa furaha. Mara moja anamrukia ili kumpokea kwa bashasha. Mama amechoka. Amekuwa na siku ndefu kazini. Haonekani kuwa mchangamfu.
Rahma anauliza maswali mengi kwa mama yake. Hajibiwi, hata pale anapojibiwa, mama haonekani kuwa na uzingativu. Ili apate nafasi ya kumpumzika, mama anamwelekeza Rahma kwenda kufanya kazi za shule alizokuja nazo nyumbani. Rahma anavunjika moyo lakini analazimika kuondoka.
Baada ya muda mfupi, wageni wanaingia. Ni rafiki zake mama Rahma. Ingawa amechoka, analazimika kuwachangamkia, mazungumzo ya mama na wageni yanapambwa na vicheko, utani na uchangamfu.
Mama anamwita Rahma awaletee wageni vinywaji. Rahma yuko mezani, anajifanya hasikii. Mama anaita kwa mara nyingine, Rahma anakuja bila kuitika. Hasalimii wageni na haonekani kujali. Mama anajisikia kudhalilika, anavumilia kwa heshima ya wageni.
Wageni wanapoondoka, mama anamrudia Rahma kwa hasira. Anamkemea kwa kuonesha utovu wa nidhamu tena mbele ya wageni wake muhimu. Rahma hajibu chochote. Mama anaamua kumchapa, Rahma anakwenda kulala huku akilia.
Wakati mwingine tunawaadhibu watoto pasipokujua kwanini wamefanya kile walichokifanya. Rahma alitamani kuwa karibu na mama yake. Alipokosa ukaribu huo, hakuitika mama yake alipomwita akiamini kufanya hivyo kungemstua mama kuchukua hatua za kurejesha ukaribu, haikuwa kama alivyotarajia.
Wakati mwingine, mtoto hukosa adabu kwa sababu tu anajisikia hawezi kufanya anachotamani. Mazingira yanapomfanya aamini hawezi, ndani yake kunajengeka msukumo wa kujaribu kuthibitisha kuwa bado anaweza.
Mtoto ana uwezo mdogo wa kuelewa na kutafsiri mambo. Namna mtoto anavyotafsiri mambo, sivyo sisi watu wazima tunavyofanya. Kufikiri mtoto anaweza kuona mambo kama vile tunavyoyaona sisi, si sahihi. Hiyo haimaanishi tupuuze hisia za mtoto, la hasha! Tunapopuuza hisia hizo hata kama ni potofu tunakuza tabia zisizofaa.
Mama yake na Rahma, kwa mfano, hakusumbuka kuelewa tafsiri ya mwanawe. Hakuwa na habari kuwa mwanawe alikuwa anajaribu kuelewa kwanini mama hajanichangamkia lakini wageni walipokuja aliwachangamkia. Mama Rahma hakufikiri mambo madogo namna hiyo.
Lakini kwa mtoto kama Rahma, hilo ni suala kubwa. Akili yake haifikirii kwa mantiki anayoitumia mama. Muda wote ufahamu wa mtoto hufanya kazi ya kutafsiri, kutengeneza hisia, kuamua na hatimaye kufanya kitu kinachokwenda sambamba na tafsiri potovu aliyoitengeneza, hisia potovu alizonazo na uamuzi potofu alioufanya. Hayo yote kwa pamoja ndiyo yanayochochea utovu wa nidhamu.
Rahma hakuamua kunyamaza kwa makusudi. Alipompokea mama yake, alikuwa na matarajio fulani. Alitegemea mama yake angemchangamkia, labda angembeba, angembusu na kumkumbatia. Mama hakufanya hivyo. Kwamba hajafanya hivyo, haimaanishi mama hampendi Rahma. Hapana. Moyoni mwake Rahma ni mtu wa thamani hata kama hajambeba, hajambusu, hajamwambia anampenda na hajamkumbatia.
Lakini kwa Rahma, ‘Kama hujafanya lolote kati ya hayo, hunijali!’ Hii ni tafsiri potofu inayojengwa na akili za kitoto. Wageni walipoingia, mama alilazimika kuchangamka. Rahma anachunguza, “kwanini mama amekuwa mchangamfu wageni walipoingia?” Anajisikia vibaya moyoni. “Mama hanijali, haoni thamani yangu.” Hizo ni hisia potofu zinazotokana na tafsiri potofu.
Hisia hizi zinamfanya Rahma afanye uamuzi. “Nitamuumiza kidogo na yeye.” Hiki ni kisasi. Mama yake anapomwita, Rahma anafanya kama alivyoamua. Ananyamaza. Mama yake hajaweza kutafsiri kwanini Rahma anafanya hayo anayoyafanya.