25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

BAHARI, MAZIWA HUTUMIKA KAMA VYOO VYA KUDUMU AFRIKA – 5

KAMA ndio mara yako ya kwanza kusoma makala hii, huu ni muendelezo wa makala ya Ufukwe wa Matema, ambapo mwandishi aliutembelea na kujionea mambo mbalimbali ya kuvutia na kustaajabisha.

Ufukwe huu umezungukwa na miamba, lakini pia watu waishio maeneo jirani hufanya shughuli zao za hapa na pale ikiwamo kufua na kuanika mazao ya nafaka. Kujua zaidi yaliyopo na yanayojili katika Ufukwe wa Matema endelea kusoma makala hii kila alhamisi na Ijumaa.

Miamba ya Mto Mwalalo

Mwanamazingira yeyote au mtu mwenye udadisi anayetembelea bonde la Mto Mwalalo kutoka mwanzo hadi kwenye maporomoko ya Mwalalo hatakosa kuvutiwa na aina mbalimbali za miamba na mawe yaliyo katika bonde hilo. Picha nilizochukua za mawe na miamba hiyo zilipelekwa kwa majiolojia waandamizi, waliobobea katika fani hii muhimu, na wenye uzoefu wa miaka mingi katika kazi, na kuwaomba maelezo kuhusu miamba ya Mto Mwalalo. Maelezo yafuatayo yametolewa na Ndugu Asa Mwaipopo na Dr. Dalaly Kafumu: “Bonde la Mto Mwalalo, Matema lina mpangilio wa mawe wa upekee fulani na unavutia.

Kijiolojia, miamba hii inaonesha kuwa na sura (lithology) kubwa mbili, lakini zote zikiwa na chembechembe ndogo ndogo. Moja ni aina ya “granite” ambayo ni aina maarufu ya mawe yanayopatikana upande wa Ziwa Victoria, hasa Mwanza na ya pili ni “delorite’’ mawe ambayo ni matokeo ya volkano iliyotokea baadaye na ambayo majivu yake yenye joto kali (lava) yalijipenyeza (cross cutting veins) kwenye miamba iliyotangulia. Miamba ya Mto Mwalalo inaonesha matukio ya kijiolojia; kuanzia mwagiko la kivolkano la awali na baadaye tetemeko au mmeguko wa ardhi uliochangia kuwapo kwa nyufa ambazo zilijazwa na lava ya volkano iliyotokea miaka mingi baadaye, na lava ilipopoa ikatengeneza mkondo mithili ya mishipa (veins) katika miamba ya awali.

Miamba inayopatikana Mto Mwalalo (granite na dolerite) huwa haina vyanzo vya madini yenye thamani (precious metals) au madini mengine ambayo kiasili hupatikana kwa wingi na kirahisi ardhini. Hata hivyo, kama mwamba una chembechembe ndogo ndogo na ni mkubwa na hauna nyufa nyingi, unaweza kutumika katika uchimbaji wa mawe ya kuchonga (dimensional stones). Mawe hayo (cut and polished stones, slabs) hutumika katika ujenzi.
Miamba ya Mto Mwalalo inaweza kuwa na sifa za kuwa mgodi wa mawe ya kuchonga (dimensional stone) kama ni miamba mikubwa, endelevu na isiyokuwa na nyufa nyingi. Ili mgodi uwezekane, unahitajika utafiti wa kjiolojia na uchorongaji ili kujiridhisha na uwezekano huo. Aidha, kwa kuwa miamba hii ipo katika bonde la mto, tathmini ya athari kwa mazingira itahitajika.
Pamoja na yaliyotangulia, eneo hili inabidi lifanyiwe uchunguzi wa kijiolojia, wanafunzi wa jiolojia, jiografia, mazingira na wengine wahamasishwe kutembelea eneo hilo na litangazwe kuvutia watalii.

 

Lyulilo
Lyulilo ni kitongoji cha Kijiji cha Ikombe, kilichopo ghuba ndogo inayoashiria mwisho wa Ziwa Nyasa unapoambaa mashariki kutoka kusini kwenda kaskazini. Ghuba hiyo imekaa kimkakati.

Ufukwe wake ni mchanganyiko wa mchanga na mawe madogo. Ufukwe uko kwenye kina kirefu kiasi kwamba meli kubwa kama vile MV Songea inayosafirisha abiria na mizigo hutia nanga mita 200 hivi kutoka sokoni Lyulilo.

 

Lyulilo ni soko maarufu kwa samaki wa Ziwa Nyasa na kwa vyungu na bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi. Mitumbwi na boti hutia nanga Lyulilo zikisafirisha vyungu kutoka Ikombe na bidhaa kwenda Ikombe.
Umaarufu wa Lyulilo unatokana na kuwa soko la vyungu vya asili vinavyotokana na udongo wa mfinyanzi. Si rahisi hasa kwa vijana wetu waliokulia mjini kufahamu umuhimu wa vyungu hivi. Kwani vijana wa zamani tunakumbuka jinsi mama zetu, shaangazi zetu na bibi wazaa mama au baba jinsi walivyotumia vyungu hivi kupikia na jinsi chakula kilichotoka humo kilivyokuwa na ladha na utamu wa aina yake. Lakini pi tunakumbuka jinsi ambavyo vyungu hivi vilitumika kama jokovu. Kwa kuweka chungu kilichojaa maji juu ya mafiga matatu na kuweka mchanga chini ya chungu na kunyunyizia maji mchanga huo, maji yaliwea kupoa na kuwa ya baridi kana kwamba yametoka kwenye jokofu.

Mnada wa vyungu hufanyika jumamosi. Hata hivyo, mauzo ya samaki, vyungu, mchele, ndizi na bidhaa nyingine hufanyika kila siku.

Halmashauri ya Wilaya ya Kyela imejenga soko la samaki kwa matarajio ya ongezeko la biashara. Soko hilo lenye majokofu ya kutunzia samaki halitumiki. Kwani umeme haujafika Lyulilo.

 

Ikombe
Moja ya vivutio vikubwa kwa wageni na watalii wanaofika Matema ni kitongoji cha Ikombe kilicho katika Kijiji cha Ikombe katika kata ya Matema. Kitongoji cha Ikombe kiko kando kando ya Ziwa Nyasa kwenye mitelemko ya Milima ya Livingstone. Ni kitongoji cha mwisho kusini mwa Matema kinachopakana na Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe. Ikombe ni peninsula au rasi ndogo inayoingia Ziwa Nyasa. Haifikiki kwa urahisi kwa nchi kavu. Kwani miteremko ya milima Livingstone ni mikali. Barabara inajengwa, yanahitajika madaraja kukamilisha ujenzi huo. Baadhi ya watalii hupenda kutembea kwenda Ikombe. Njia rahisi kwa sasa kufika Ikombe ni kutumia boti, safari inayochukua dakika 20. Wenyeji hutumia ngalawa kwa usafiri na kupeleka bidhaa mbalimbali Ikombe.

Ras ya Ikombe ina mvuto wa kipekee. Ufukwe wake ni wa mawe madogo na kawaida. Ufukwe umejaa ngalawa. Ikombe ni kijiji cha wavuvi, usafiri wa kwenda sehemu nyingne za Kata ni wa kutumia ngalawa. Madhari ya kitongoji inapendeza kutokana na miti mingi ya asili na iliyopandwa inayoipa Ikombe tabianchi ya kipekee. Hapa ndipo vyungu vya asili hutengenezwa na huvushwa kwa mitumbwi kupelekwa Lyulilo kuuzwa. Udongo mfinyanzi unaopatikana Ikombe ndio unaofaa kutengeneza vyungu. Ikombe pana zahanati na shule ya msingi.

 

Huduma za kijamii
Baada ya kuugua kwa muda mrefu na kutibiwa India na hapa nchini kati ya mwaka 2011 na 2013 kila ninapoulizwa kipaumbele cha maendeleo kiwe nini, hasa pale ambapo rasilimali ni kidogo, huwa najibu afya na elimu. Kabla ya hapo jibu langu lilikuwa elimu na elimu tu. Kwa upande wa Matema, suala la afya linaweza kugawanywa katika sehemu mbili; elimu ya usafi wa mazingira na tiba.
Maeneo ya mwambao wa maziwa na bahari barani Afrika bado yana changamoto kubwa inayohusu usafi wa mazingira, maneno ya kistaarabu yanayomaanisha uwepo au la wa vyoo. Jamii nyingi, vijijini na mijini katika mwambao wa maziwa na bahari hutumia bahari na maziwa kama vyoo vya kudumu. Nilipotembelea Pangani nikiwa Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Mazingira, nilikumbana na changamoto mbili. Kwanza, mji huo wa kihistoria ulikuwa unaharibiwa na mawimbi ya bahari yaliyokuwa yakimeza ufukwe pole pole na kuharibu nyumba na miundombinu kwa sababu ya kiwango kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi.
Changamoto ya pili ilikuwa ni uhaba wa vyoo. Jamii ilikuwa ikienda ufukweni mwa bahari ili kujisaidia, ilitupa taabu ya kukagua uharibifu wa pwani ya Pangani, ilitubidi kukagua eneo lote kwa kutembea ufukweni na kila mara kuruka kinyesi. Nilipata changamoto ya aina hiyo Mikindani, Lindi. Ukikaa katika hoteli nzuri ya kitalii na ukiwa makini unaweza kugundua kuwa makazi mengi ya Mikindani hayana vyoo, wakazi wa eneo hilo hutumia Bahari ya Hindi kama eneo la kutimiza wito asilia. Pangani na Mikindani ni miji midogo.
Kuna wakati nilienda Accra, Ghana kuhudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Kama ilivyo kawaida yangu, alfajiri huwa natoka hotelini ili kufanya mazoezi ya matembezi. Umbali kidogo kutoka hoteli ya kitalii niliyokaa kuna ufukwe wenye mchanga na mawe. Nililoliona na lililonishangaza ni kwamba jamii kutoka kitongoji cha jirani walishuka ufukweni kila asubuhi kwa kile nilichodhani wanaenda kuoga au kuogelea. Haikuwa hivyo, walikuwa wamekaa tu. Nilipouliza nini kilikuwa kinaendelea, wahudumu pale hotelini wakaniambia kuwa wale wote niliowaona walikuwa wameenda baharini kujisaidia.

Itaendelea kesho…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles