22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

NYUMBA ZISIZO NA VYOO ZAWEKWA BENDERA NYEKUNDU KUASHIRIA HATARI

Na ELIUD NGONDO, NJOMBE


SERIKALI imedhamiria kuboresha vyoo katika maeneo ya mijini na vijijini, lengo likiwa ni kuepuka maambukizi ya magonjwa yatokanoyo na uchafu wa vyooni.

Ili kutekeleza azma hiyo, taasisi isiyo ya kiserikali ya Sanitation And Water Action (SAWA) imekuwa ikielimisha na watu juu ya umuhimu wa kujenga vyoo bora na vya na kisasa katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe.

Mhandisi Mshauri wa taasisi hiyo, Wilhelmina Malima anasema licha ya kuwaelimisha juu ya umuhimu wa vyoo vya kisasa, pia wamekuwa na mradi wa kuwajengea tangu mwaka juzi.

Malima anasema kabla ya kuanza utekelezaji wa mridi wa ujenzi wa vyoo vya kisasa, waliuona uongozi wa Wilaya ya Makete ambao uliwataka waanze kutekeleza katika bonde la Matamba ambako kuna kata tano, vijiji 17 na vitongoji 79.
Anasema wakati mradi huo unaanza, wananchi wengi walikuwa wakitumia vyoo vya mashimo vilivyowekwa mabanzi hali iliyokuwa ikihatarishamaisha yao.

Mhandisi Wilhelmina anasema baada ya kuona hivyo, waliamua kuelimisha wananchi juu ya madhara ya kutokuwa na vyoo na kuwashauri kuviboresha walivyokuwa wakitumia awali na baadaye wachimbe vya kudumu.

“Hali ilikuwa mbaya kwa wananchi, lakini baada ya kuwaelimisha, wananchi wengi sasa wamechimba vyoo bora na vya kisasa, hivyo magonjwa ya kuhara yamepungua kwa asilimia kubwa,” anasema Mhandisi Wilhelmina.
Anasema mradi huu pia unadhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), ambao wanawezesha kuwafikia watu wengi zaidi katika taasisi, shule na makanisa.
Anasema lengo ni kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora.

“Shuleni huwa tunajenga vyoo bora vyenye huduma zote muhimu kama maji ili mtoto aweze kujitawaza na kunawa mikono kwa kutumia sabuni. Pia tunajenga vyoo maalumu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.
Mhandisi huyo anataja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni pamoja na wananchi kuwa wagumu kuwaelewa kwa sababu ya kuzoea kutumia vyoo vya mashimo vyenye mabanzi.
“Jamii ilikuwa imeshazoea kutumia vyoo vya mabanzi na wengine kujisaidia vichakani hivyo kuwahamasisha ilikuwa ni kazi ngumu.

Ofisa Afya Wilaya ya Makete, Bonifas Sanga anasema SAWA wamesaidia kwa kiasi kikubwa kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujenga vyoo bora na vya kisasa, hali ambayo imesaidia baadhi ya vijiji wilayani Makete kuingia katika mashindano ya kitaifa ya ujenzi wa wa vyoo bora.

VIJIJI VINAVYOSHINDANA

Sanga anataja vijiji vilivyoingia katika ushindani wa vyoo bora kitaifa na nafasi yake kwenye mabano, kuwa ni Makusi iliyoshika nafasi ya sita, Mpangala (10) na kijiji cha Magoye (17).

Anaeleza kuwa mchango mkubwa wa Serikali kwa wananchi ni kuweza kuhakikisha kunakuwepo na huduma ya maji ambayo yatasaidia wananchi wanapoenda kujisaidia kuwa na maji safi na salama.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makusi, Yonam Msigwa anasema sasa hivi vyoo ambavyo havina ubora kijijini hapo ni vitatu tu, watu wameelimika.

VYOO NA IMANI ZA KISHIRIKINA
Wananchi wengi wa vijijini wanaamini kuwa kushika choo wakati wa kujisafisha baada ya kujisaidia ni ushirikina, kwa sababu ukitoka chooni utasalimiana na watu kwa kushikana mikono.
Sasa basi, kabla ya elimu kutolewa wengi wao walikuwa wanaona kinyaa kujitawaza mara baada ya kujisaidia, hivyo walikuwa wakijisaidia vichakani.

Mwenyekiti huyo anasema baada ya kuelimishwa, vinyesi vilivyokuwa vikitapakaa kila eneo havipo tena.
Anasema ujenzi wa vyoo bora umesaidia kupunguza maradhi na hivyo wananchi kufanya shughuri za uzalishaji na kujiongezea kipato.

 

UMEBORESHA ELIMU
Mkuu wa Shule ya Sekondari Matamba, Yula Sanga anasema ujenzi wa vyoo bora umechangia wanafunzi kuhudhuria masomo kila siku.
Anasema wanafunzi wamekuwa mabalozi wazuri wa kuimarisha usafi mara baada ya kutoka chooni kwa kuhakikisha wananawa mikono kabla ya kuingia darasani.

VYUMBA MAALUMU VYA WASICHANA VIMEPUNGUZA UTORO
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Magoye, Isso Mwinuka anasema sasa hivi wanafunzi waliopevuka wana chumba chao maalumu kwa ajili ya kujistiri pindi wanapokuwa katika siku za hedhi.
Anasema hali hiyo imepunguza utoro shuleni kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wanafunzi wa kike huwa na amani hata wanapokuwa kwenye siku zao, tofauti na awali ambapo wakiwa kwenye hedhi hulazimika kukaa nyumbani kwa kuepuka kukosa namna ya kujisitiri.

MAGONJWA YAPUNGUA
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Matamba, Braiton Ndandala anasema SAWA wamesaidia kupunguza magonjwa ya kuhara.
Anasema mwaka 2015 kesi za wananchi kukabiliwa na magonjwa ya kuhara, kuhara damu na homa ya matumbo zilikuwa nyingi tofauti na sasa.

“Julai mwaka 2015 hadi Juni 2016 wagonjwa wa kuhara walikuwa 898 na mwaka Juni 2016 hadi Julai 2017 wagonjwa walikuwa 256; idadi ambayo imepungua tofauti na awali.
“Kuwapo kwa mradi huu kumepunguza mno tatizo la magonjwa haya, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma,” anasema Dk. Ndandala.
Maratibu wa Mradi wa Uhamasishaji ujenzi wa vyoo, Kelvin Mwanshilo anasema wamejiwekea utaratibu wa kuzunguka nyumba hadi nyumba kuhakikisha wananchi wanajenga vyoo bora.


NYUMBA KUWEKEWA BENDERA NYEKUNDU

Mratibu huyo anasema walizungumza na viongozi wa kata, vijiji na vitongoji na kukubaliana kuwa kila nyumba ambayo haijamaliza ujenzi wa choo bora iwekewe bendera nyekundu.
Anasema hiyo imesaidia kuchochea wananchi kujenga vyoo bora kwani wamekuwa wakichekwa na wenzao waliokamilisha ujenzi.
Akizungumzia faida za vyoo bora, mkazi wa wa Kijiji cha Makusi, David Mbilinyi anasema sasa hivi hawaumwi ovyo magonjwa yanayosababishwa na uchafu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles