25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU YA UHAMIAJI KUANZA KUTOA VIZA

Na LEONARD MANG’OHA


KABLA ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, mwaka 1914-18 udhibiti wa wageni nchini haukuwa muhimu, lakini baada ya vita hiyo ilionekana lazima kuwapo utaratibu wa uingiaji wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Hapo ndipo suala la Viza likaanza kutumika kama nyenzo kuu ya udhibiti wahamiaji, na ilitolewa ili kudhibiti uingiaji na utokaji katika koloni la Tanganyika kwa lengo la kulinda maslahi ya wakoloni wenyewe.

Utaratibu wa utoaji wa Viza ulizingatia uhusiano uliokuwapo kati ya wakoloni na taifa husika. Lengo kuu lilikuwa ni kuzuia uingiaji holela wa wageni, hususan wageni waliokuwa na makoloni katika maeneo mengine ya Afrika kama Wafaransa, Wabelgiji, Wajerumani na mataifa mengine.

Kutokana na mahitaji ya manamba katika mashamba ya wakoloni, raia wengi wa Afrika walikuwa huru kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kurahisisha upatikanaji wa wafanyakazi.

Utaratibu wa utoaji vibali vya ukaazi Tanganyika uliwekwa ili kusaidia utawala wa kikoloni kudhibiti ukaazi wa raia wa mataifa mengine adui. Utaratibu huo haukuwahusisha Waafrika isipokuwa makabila ya Wakikuyu, Wajaluo na Wakamba kutoka nchini Kenya kutokana na msimamo wao katika harakati za kudai uhuru.

Utaratibu wa utoaji vibali vya ukaazi umekuwa ukibadilika kulingana na mabadiliko ya kiutawala kuanzia enzi za ukoloni hadi Uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ulipopatikana mwaka 1961  na 1963 na baadae Muungano mwaka 1964.

Utaratibu wa kutoa vibali hivyo ulianza kutumika mwaka 1924 baada ya kuundwa kwa sheria ya Uhamiaji namba 37 ya mwaka 1924. Kwa mujibu wa sheria hiyo, wageni wa mataifa mengine (wasio Waingereza), walilazimika kupewa leseni za kuingia na kuishi.

Wageni waliokuwa wakisamehewa ni watumishi wa serikali, waliokuwa na hadhi ya kibalozi na wanajeshi.

Kuundwa kwa Sheria ya Uhamiaji 50 ya mwaka 1947 iliyofuatiwa na sheria nyingine ya Uhamiaji ya mwaka 1948 kulileta mabadiliko katika utaratibu wa utoaji wa vibali vya ukaazi.

Baada ya sheria hiyo, vibali vya leseni vilikoma na kuanzishwa utaratibu wa vibali vya ukaazi wa kudumu, ambapo hati ya ukaazi daraja A ilitolewa kwa mtu aliyekuwa na hati ya ukaazi ya kudumu.

Pia hati hii ilitolewa kwa mtu aliyewasilisha kwa Ofisa Uhamiaji hati halali ya ukaazi ya kudumu iliyotolewa na serikali ya koloni ya Kenya, Tanganyika na Uganda, ambayo ilionesha kwamba alikuwa raia katika moja ya makoloni hayo au ni mtoto wa mtu yeyote ambaye ni mkaazi katika makoloni husika au mfanyakazi wa Serikali.

Mtu yeyote aliyepewa kibali cha kuingia nchini, ikiwa hakuingia katika kipindi cha mwaka mmoja, kibali chake kilikoma kutumika, hivyo kulazimika kuongezewa muda na ofisa uhamiaji mkuu alipewa mamlaka ya kuongeza kibali hicho kwa kipindi cha miaka miwili ikiwa aliona inafaa.

Hati ya ukaazi daraja B ilitolewa kwa watu waliokuwa na leseni kutoka sekta za kilimo, mifugo na biashara kwa sharti kuwa awe amepata, au ana ruhusa ya kupata ardhi katika eneo linalofaa kwa biashara anayopendekeza kuifanya, awe na mtaji wa Sh 16,000 au chini ya hapo kadiri bodi itakavyoamua.

Katika hati ya ukaazi Daraja C, mtu ambaye bodi ilimpatia cheti kwamba imeridhika mtu huyo ni mwajiriwa, mfanya utafiti wa madini au mchimbaji.

Hati ya ukaazi daraja D ilitolewa kwa mwombaji ambaye bodi ilimpatia cheti kuonesha kwamba imeridhika mtu huyo anafanya biashara makoloni ya Kenya, Uganda na Tanganyika, au mwajiriwa.

Hati daraja E, kwa mtu ambaye ni mzalishaji mali viwandani wakati daraja F ilitolewa kwa raia wa kigeni waliokuwa na utalaamu wa ukaguzi hesabu na wahasibu waliokuwa na sifa za kutosha.

Daraja G ilitolewa kwa mfanyakazi wa kuajiriwa katika sekta mbalimbali kwa mkataba wa muda mrefu.

Kanuni namba 20 ya kanuni za uhamiaji ilianzisha pasi ya muda ya ajira, hati ya ufuasi pasi ya muda ya ajira hati ya mwanafunzi, hati maalumu na hati ya matembezi.

Baada ya Uhuru, Tanganyika na Zanzibar ziliendelea kurithi mfumo wa kikoloni wa utoaji vibali vya ukaazi kwa wageni hadi ilipoanzishwa sheria namba 41 ya mwaka 1963 iliyoanzisha kutolewa kwa vibali vya daraja A na B tu, utaratibu ambao unaendelea hadi sasa.

MWISHO.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles