25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

BARIDI HAISABABISHI NIMONIA KWA WATOTO – DAKTARI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


NOVEMBA 12, mwaka huu Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Nimonia Duniani.

Nimonia ni miongoni mwa magonjwa yanayotajwa kuchangia idadi kubwa ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Unatajwa kuwa ugonjwa hatari unaoathiri mapafu ya binadamu ukishambulia watu wa rika zote.

Hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa watoto ndiyo walio katika hatari ya kupoteza maisha kuliko watu wazima.

Kaimu Meneja Programu ya Afya ya Mtoto wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Felix Bundara anasema hiyo ni kwa sababu kiwango chao cha kinga ya mwili kupambana na magonjwa mbalimbali huwa kidogo tofauti na ilivyo kwa watu wazima.

“Miili ya watoto huwa bado haina kinga ya kutosha kupambana na magonjwa mbalimbali ikiwamo nimonia, ndiyo maana anapougua ikiwa hajapatiwa matibabu sahihi ni rahisi kupoteza maisha,” anabainisha.

Anasema mtu hupata ugonjwa huo kutokana na maambukizi ya wadudu (bakteria), fangasi au virusi.

 

Hali ilivyo

Dk. Bundara anasema tafiti zinaonesha ugonjwa huo ni tishio si tu Tanzania bali duniani kote, ukichangia idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga.

Anaongeza: “Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015/16 (TDHS) unaonesha kati ya vifo 100 vya watoto wachanga vinavyotokea nchini vifo 15 kati yake huwa vimetokana na ugonjwa huu wa nimonia.

Anaongeza: “Tafiti zinaonesha pia ugonjwa huo unashika nafasi ya pili nchini kati ya magonjwa yanayosababisha idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga.

 

Changamoto

Dk. Bundara anasema kwa mujibu wa utafiti huo wa TDS unaonesha wazazi na walezi wengi huwa hawawepeleki watoto wao hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa mapema pindi wanapopata kikohozi.

“Hali hiyo watoto kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha ikiwa wanasumbuliwa na nimonia na wakakosa matibabu sahihi mapema,” anasema.

Anasema utafiti huo unaonesha kati ya watoto 100 waliopata kikohozi wakati wa kipindi hicho, 55 pekee ndiyo waliofikishwa hospitalini kwa matibabu.

“Watoto 45 haijulikani wanaishia wapi, sasa hii ni changamoto kubwa katika kukabiliana na ugonjwa huu, jamii inapaswa kuamka na kuhakikisha mtoto anapopata tatizo la kikohozi anafikishwa mapema hospitalini kwa uchunguzi.

“Wapo pia wazazi na walezi waliojenga utamaduni wa kwenda wenyewe katika maduka ya dawa na kununua dawa za ‘antibiotics’ na kuwapatia watoto wanapopata kikohozi.

“Si jambo sahihi, wajue kwamba si kila kikohozi ni nimonia kitendo cha kuwapatia dawa bila ushauri wa daktari kinaweza kusababisha kutengeneza usugu wa dawa mwilini,” anasisitiza.

 

Dalili

Daktari huyo anasema dalili kuu ya kwanza huwa ni kukohoa au kupumua kwa shida au vyote viwili kwa pamoja.

“Yaani unakuta anakohoa au anapumua kwa shida, lakini nisisitize si kila kikohozi ni nimonia, inahitaji uchunguzi wa kina ili uweze kujua kwamba ni nimonia au la kwa sababu matibabu yake yanatofautiana.

“Kuna mtoto anaweza kuletwa hospitalini akiwa na tatizo la kikohozi akichunguzwa kasi yake ya upumuaji daktari anakuta haijaongezeka na ipo kawaida kabisa.

“Hivyo, matibabu ya mtoto wa aina hii huwa hapewi ‘antibiotics’ badala yake anapewa ‘vitulizo salama’ na kama ananyonya basi anaendelea kunyonya maziwa ya mama yake kama kawaida.

“Hata ikiwa ameanza kula vyakula mbalimbali ataendelea kula kama kawaida lakini atalazimika kupatiwa chai ya asali na limao kwa maelekezo maalum ya daktari ili kutibu tatizo lake,” anabainisha.

Anaongeza: “Mtoto mwingine anaweza kuletwa hospitalini na akagundulika ana nimonia lakini si ile kali, huyu unakuta anakohoa na kasi yake ya upumuaji imeongezeka.

“Lakini hii huwa inatofautiana pia, watoto wenye umri wa mwaka sifuri hadi miezi miwili kwa kawaida ukihesabu kasi yao ya upumuaji haitakiwi iwe 60 au zaidi, ikiwa tofauti na hapo na anakohoa daktari anajua hiyo ni nimonia.

“Kwa watoto wenye umri wa miezi miwili hadi miezi 12 kasi yake ya kupumua haitakiwi kuwa 50  au zaidi ukikuta ni tofauti na kiwango hicho na anakohoa tunasema hiyo ni nimonia.

“Watoto wa miezi 12 hadi miezi 59 kasi yao ya upumuaji haitakiwi kuwa 40 au zaidi ikiwa tofauti na kiwango hicho tunajua hiyo ni nimonia.”

Daktari huyo anasema ikiwa kasi ya upumuaji imezidi viwango hivyo moja kwa moja wanajua hiyo ni nimonia, kwamba matibabu yake kwa kawaida huwa ni kumpatia mgonjwa vidonge vya amoxilline kwa maelekezo maalumu ya daktari.

“Lakini unaweza kupokea mtoto ambaye anakohoa na kasi yake ya upumuaji imeongezeka kuliko kawaida, aidha, unakuta ana historia ya kutapika, degedege, amelegea mno mwili wake au amepoteza fahamu basi moja kwa moja tunajua hiyo ni nimonia kali,” anasema.

Dk. Bundara anasema mgonjwa mwenye dalili hizo anapaswa kuwahishwa hospitalini ili apatiwe matibabu sahihi kuokoa maisha yake.

“Sambamba na dalili hizo, unaweza kukuta pia anapata shida ya kubanwa kifua au katika sehemu ya chini ya kifua unakuta inaingia kwa ndani pindi anapopumua na anapopumua unakuta anatoa sauti fulani, hizo pia ni dalili ya nimonia kali,” anabainisha.

 

Mazingira hatarishi

Daktari huyo anasema wapo watu ambao huamini kwamba kitendo cha mtu kuishi katika maeneo yenye baridi kali moja kwa moja humuweka kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo lakini si kweli.

“ Ingawa kuna baadhi ya tafiti (sayansi) ambazo inaonesha mazingira ya baridi ni hatarishi kwani wale wadudu wanaweza kuzaliana kwa wingi lakini si sababu ya msingi mno kwamba watu wanaoishi katika maeneo hayo huathirika zaidi kuliko maeneo mengine,” anasema na kuongeza:

“Watoto wakiwekwa katika mazingira ya moshi, yaani unakuta watu wanapikia ndani na kuna moshi labda unaotokana na kuni, mkaa au sigara, moja kwa moja mtoto huwa kwenye hatari ya kupata tatizo hili.

“Lishe ni jambo la muhimu pia katika kumkinda mtoto kupata tatizo hili hasa inayotokana na maziwa ya mama humuepusha mtoto dhidi ya ugonjwa huu,” anabainisha.

 

Mafanikio ya chanjo

Anasema licha ya changamoto iliyopo kwa baadhi ya wazazi na walezi kutowafikisha watoto wao mapema hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu, serikali imeendelea kujitahidi kuwapatia chanjo wale wanaofikishwa hospitalini kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo.

“Matokeo ya Utafiti wa ‘Global Action Plan for Nimonia’ uliotolewa mapema mwaka huu ambapo takriban nchi 20 tulifanyiwa ufuatiliaji, Tanzania imeongoza kwa asilimia 90 katika utoaji chanjo dhidi ya nimonia,” anabainisha.

Anasema huduma hiyo inatolewa nchi nzima hasa katika vituo vyote vinavyotoa huduma ya mama na mtoto.

Anasema licha ya matokeo haya yaliyoonesha mafanikio, bado tunahitaji kuihamasisha jamii kuhakikisha watoto wanafikishwa mapema hospitalini ili kufikia kiwango cha asilimia 100.

“Ni muhimu mtoto afanyiwe uchunguzi, nasisitiza kwamba si kila kikohozi ni nimonia inahitaji uchunguzi kujua kwa sababu matibabu yake yanatofautiana na ikiwa atapatiwa dawa kiholela ni hatari zaidi,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles