24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

YAFANYE MAZOEZI KUWA TABIA UKABILIANE NA MARADHI

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD


WATU wengi tunafahamu umuhimu wa mazoezi katika kulinda afya zetu. Licha ya ufahamu huo, huenda tukawa hatufahamu ni mazoezi yapi tufanye ili yatusaidie katika miili yetu. Leo tutajadili matatizo makubwa matano ya kiafya yanayoweza kutukabili na aina ya mazoezi yanayofaa kukabiliana nayo.

 

Magonjwa ya moyo na mishipa

Katika kundi hili kuna magonjwa ya moyo na matatizo kama vile kupanda kwa shinikizo la damu (pressure). Kuzuia matatizo haya inatupasa kufanya mazoezi ya aerobics angalau mara tano kwa wiki. Mazoezi ya aerobics ni pamoja na kutembea, kukimbia, kuogelea na kuendesha baiskeli. Kucheza muziki (aerobic dancing) ni aina hii ya mazoezi pia. Hakikisha unafanya mazoezi hayo kwa muda usiopungua nusu saa. Kumbuka pia kufanya mazoezi ya nguvu (kunyanyua au kusukuma uzito) angalau mara tatu kwa wiki. Usisahau pia kufanya mazoezi ya kulainisha na kunyoosha viungo (flexibility exercises). Kufaidika fanya mazoezi haya kuwa tabia.

 

Ugonjwa wa kisukari

Mazoezi ya aerobics pia ni muhimu katika kuzuia ugonjwa wa kisukari. Mazoezi ya nguvu ambayo huipa misuli nguvu ni muhimu pia katika kuzuia ugonjwa wa kisukari. Sukari inayoingia katika mwili hutumiwa kwa kiasi kikubwa na misuli na mazoezi huipa misuli uwezo wa kutumia sukari zaidi. Hii huzuia sukari isiongezeke katika damu. Kuzuia kabisa tatizo hili fanya mazoezi kuwa tabia.

 

Maumivusuguyamgongo

Kuzuia tatizo hili mazoezi ya kulainisha na kunyoosha viungo ni muhimu. Kumbuka kwamba wengi wetu tunafanya kazi zinazotulazimu kukaa kwa kipindi kirefu. Kwa maana hiyo ni muhimu kujinyoosha mara kwa mara ili kuzuia kukakamaa kwa viungo, kitu ambacho huchangia kusababisha maumivu sugu ya mgongo. Hakikisha unajinyoosha kila baada ya kukaa kwa saa moja mfululizo. Usiruhusu kukaa kwa zaidi ya saa moja bila ya kujinyoosha. Fanya mazoezi ya kunyoosha mgongo angalau mara tatu kwa wiki na usisahau kufanya mazoezi ya aerobics kama vile kutembea.

 

Maumivu sugu ya magoti na maungio mengine

Kama ilivyo kwa maumivu sugu ya mgongo, maumivu sugu ya magoti na maungio mengine huchangiwa na ukosefu wa mazoezi ya kulanisha na kunyoosha viungo. Kutokufanya mazoezi haya husababisha maungio kama vile magoti, nyonga na mabega kukakamaa na kusababisha milipuko ya kibaiolojia (inflammation) ambayo huleta maumivu makali. Hakikisha unafanya mazoezi haya mara kwa mara. Ni muhimu pia kufanya mazoezi haya kila unapo amka asubuhi. Tunapolala kwa muda mrefu viungo vyetu hukaa katika hali moja kwa muda mrefu, na ni muhimu kuvinyoosha ili vijiweke tayari na mishuguliko ya siku.

 

Msongo wa mawazo na matatizo mengine ya akili

Msongo wa mawazo (stress) husababishwa na kuongezeka kwa viwango vya vichocheo vya stress kwa muda mrefu. Kuongezeka kwa vichocheo hivi husababisha kupungua kwa vichocheo vya furaha na nguvu. Mazoezi kama vile kukimbia na kuogelea husaidia kuongeza kiwango cha vichocheo vya furaha na kupunguza kiwango cha kichocheo cha msongo wa mawazo (stress). Mazoezi ya nguvu kama vile kunyanyua au kusukuma uzito, huongeza kiwango cha kichocheo kinachoitwa testosterone mwilini. Testosterone huongeza nguvu mwilini na kutufanya tujiamini. Kwa pamoja mazoezi husaidia kuimarisha ufanyaji kazi wa ubongo na kutufanya wenye furaha, nguvu na ufanisi wa kufanya kazi.

Ili kujikinga na magonjwa ni sharti tufanye mazoezi mchanganyiko na tuyafanye kuwa kama tabia

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles