33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MKE WA KAFULILA AMSHANGAA MUMEWE

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


MKE wa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, Jesca Kishoa, amesema mumewe ni mtu aliyeingia kundi la wanasiasa wasio na msimamo.

Amesema sababu alizozitoa za kujiondoa upinzani hazina mashiko na zimekuwa zikitumiwa na wanasiasa wasiokuwa wapambanaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kishoa, alisema wakati wote mumewe amekuwa na msimamo usioyumba, lakini anashangazwa kaingia katika mtego mbovu.

“Namfahamu mume wangu kuliko mtu yeyote, kile alichokisema hata siamini. Mimi nilipata taarifa za Kafulila kujiondoa Chadema kama ambavyo watu wengine wamepata.

“Tangu nimekuwa naye,  sikuwahi kumwona akiisifia CCM, bali alisimamia misimamo  yake kwa dhati na bila ya kuyumbishwa na mtu yeyote.

“Yeye alikuwa Dar es Salaam na mimi nipo Dodoma na sikuwa nimeelezwa chochote na yeye juu ya uamuzi wake huu aliouchukua,” alisema.

Kishoa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, alisema kitendo cha mumewe kujiondoa katika chama hicho na kudai kuwa upinzani umepoteza ajenda ya ufisadi na kumsifu Rais Dk. John Magufuli kuwa ndiye anapambana na ufisadi, jambo si la kweli.

“Wanasiasa ambao hawana misimamo ndiyo husingizia vitu hivyo, siamini kama maneno yale yalitoka rohoni mwake, CCM si mahali sahihi kwa kuzungumzia mambo ya ufisadi hata kidogo.

“Bado naamini kuwa Chadema ni mahali sahihi kabisa ambapo siwezi kufikiri siku moja nitatoka, hivyo siyumbi kwa hilo na wanaonipigia simu watambue hilo,” alisema.

Kishoa alisema taarifa za mumewe kujiondoa Chadema amezipata kupitia vyombo vya habari akiwa Dodoma kwenye kampeni za udiwani, lakini alimpigia wakazungumza sana na bado hakumpa sababu zilizoshiba za kuondoka kwake.

Alisema wakati wote katika maisha yao, mumewe amekuwa ni muumini mzuri wa kuhubiri habari za ufisadi, ikiwamo pale alipotoa maisha yake kuhusu sakata la Escrow.

“Kila mtu anafahamu jinsi ambavyo Chadema imekuwa ndani ya ajenda ya ufisadi, tumezungumzia Lugumi, ununuzi wa ndege ambao haukufuata utaratibu, mabehewa hewa na kuibua mambo mengine makubwa, ikiwa pamoja na sakata la Escrow na CCM,” alisema Kishoa.

Alisema kuwa alichokifanya mumewe haamini kama ameamua yeye mwenyewe, ila anadhani kuna kitu kimefanya kilichosababisha kuchukua uamuzi huo.

Mbunge huyo alisema kuwa upinzani ndio ambao umekuwa ukifichua masuala mbalimbali ambayo Serikali na CCM wamekuwa wakiyatumia kama ajenda zao.

Alisema kila mmoja anafahamu jinsi Chadema ambavyo imekuwa ikipambana na ajenda ya ufisadi, huku akitolea mfano sakata la Lugumi, ununuzi wa ndege ambao haukufuata taratibu.

Kishoa alisema kwa mume wake kwenda CCM, anaamini si sehemu sahihi ya kupambana na ufisadi kutokana na kuwa na misimamo ambayo haiwezi kuendana na chama hicho.

 

HATIMA YAKE CHADEMA

Kuhusu hatima yake ndani ya Chadema, Kishoa alisema yeye hayumbishwi na chochote kutokana na kuhama kwa Kafulila, bali ataendelea kuwa mwanasiasa makini ndani ya chama hicho.

“Nitaendelea kuwa mwanachama makini wa chama changu na siyumbishwi na kuhama kwa Kafulila,” alisema.

Alisema alichokifanya mume wake ni haki yake kikatiba na yeye hawezi kuyumbishwa na msimamo wa mtu mwingine.

Hata hivyo, alidai kuwa kwa jinsi anavyomfahamu mume wake huo hauwezi kuwa uamuzi wake labda kuwe na sababu nyingine.

“Alichokifanya Kafulila ni haki yake kikatiba na mimi siwezi kabisa kuyumbishwa na msimammo wake lakini ninao uhakikia kuwa kuna sababu nyingine ambazo zimemfanya afikie maamuzi haya,” alisema.

 

POLISI NA WANAHABARI

Awali kabla ya Kishoa kuzungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema),  aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Desert Pub iliyopo Area D.

Lakini kabla mbunge huyo hajaanza kuzungumza na waandishi, waliingia askari polisi wakiwa katika magari mawili Toyota Land Cruiser na Noah na kuwafukuza waandishi wa habari waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.

Baada ya zuio hilo, iliilazimu Chadema Kanda ya Kati kuwaita waandishi katika ofisi zao zilizopo eneo la Area C ambako Kishoa alitoa ujumbe wake kwa umma.

Juzi, Kafulila, alitengeneza historia nyingine kisiasa baada ya kutangaza kuhama Chadema.

Hatua hiyo inatajwa kama historia ya aina yake kwa mwanasiasa huyo, ambaye ametumikia vyama viwili tofauti katika kipindi cha miaka 10, huku akitarajiwa wakati wowote kujiunga na chama kingine.

Kafulila alitangaza uamuzi wa kujivua uanachaa wa Chadema juzi katika taarifa yake huku akidai kwamba hana imani tena na upinzani katika kupambana na ufisadi.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Kafulila, alidai kwamba kwa sasa bado anatafakari na hivi karibuni atatangaza jukwaa jipya akimaanisha chama atakachohamia ili kuendeleza harakati zake dhidi ya ufisadi.

Akielezea sababu za kuhama chama hicho ambacho ni miezi 11 tu tangu ahamie akitokea NCCR-Mageuzi, alisema ni upinzani kukosa ajenda ya ufisadi.

Kafulila ambaye alitoka Chadema mara ya kwanza mwaka 2009 na kujiunga NCCR, alisema hiyo inatokana na Rais Magufuli kushughulikia kwa vitendo ajenda hiyo, hasa baada ya watuhumiwa na wahusika wa rushwa kubwa kufikishwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles