33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

CCM YATIKISA UPINZANI

KARIBU: Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akizungumza na wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama hicho, Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeleta mtikisiko kwa vyama vya upinzani, hasa Chadema na ACT- Wazalendo ambavyo viongozi wake wametangaza kujiunga na chama hicho tawala.

Vigogo hao kutoka upinzani, walitangaza uamuzi huo katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana mbele ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli.

Waliotangaza kujiondoa Chadema ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Patrobas Katambi na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha.

Kutoka ACT-Wazalendo ni aliyekuwa mshauri wa chama hicho ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, aliyekuwa Katibu Mkuu Samson Mwigamba, Mshauri wa Sheria, Albert Msando na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Edna Sunga.

Akizungumza katika kikao hicho, Katambi alisema upinzani wa sasa umekuwa haujadili matatizo na kuyatafutia suluhu, bali unajadili mambo binafsi.

“Leo hii nasaliti ubinafsi na umimi kwa kuamua kujiunga na CCM. Tunachosema jukwaani si kile tunachokiishi, upinzani umegubikwa na ubinafsi, umimi na makundi ya hapa na pale.

“Kijana ndani ya upinzani ni karai linalojenga ghorofa. Karai huonekana takataka baada ya ghorofa kukamilika,” alisema Katambi.

Naye Profesa Mkumbo alisema ameamua kujiunga CCM ili awe sehemu ya kuleta mapinduzi ya kiutawala, kisera, kiitikadi na ya wananchi.

“CCM kina nguvu kubwa kwa sababu ni chama cha wanachama, watu wanakiogopa chama na si chama kuwaogopa watu.

“Hata nasi tulijaribu kujenga misingi hii huko tulipokuwa upinzani, lakini tumeshindwa,” alisema Profesa Mkumbo.

Kwa upande wake, Msando, alisema kuwa anajivunia kuwa mwana CCM.

“CCM ni chama kinachoonyesha kuwajali watu, mimi kama kijana ninajivunia kuwa mwanachama wa CCM.

“CCM kiliahidi kupambana na umasikini, kutengeneza ajira, kurudisha nidhamu na uwajibikaji. Tuna kila sababu ya kupongeza kwa haya mambo mazuri.

“Nina imani sasa mnajenga chama na chini ya uongozi wa Rais Magufuli CCM mpya inapatikana. Sioni aibu kuwa CCM, kipindi cha nyuma mtu alikuwa anaogopa kusema yeye ni mwana CCM, lakini kwa sasa mtu anajivunia kwa sababu yaliyoahidiwa kwenye ilani yanatekelezwa kwa vitendo.

“Chama kiliahidi kupambana na ufisadi na rushwa, lakini sasa hivi tunaona ni watu wa aina gani wanachuchumaa mahakamani, zamani ilikuwa unaweza ukapiga simu mtu akapewa dhamana hata saa 6 usiku, lakini siku hizi haiwezekani… nidhamu na uwajibikaji unarudi,” alisema Msando.

Naye Masha alisema ameamua kurudi CCM kwa sababu ni nyumbani kwani alizaliwa ndani ya chama hicho.

“Nilipohama nilimficha baba, alinipigia na kuniuliza nimefanya nini na mimi nilimuuliza wewe uko chama gani… akasema yeye alifukuzwa na mimi nimehama, hivi ni vitu viwili tofauti.

“Nimekuja hapa kuwaombeni mnipokee mwana mpotevu nimerudi, niko imara na nitakuwa mwaminifu kwa chama na Serikali, ukinihitaji nitumie,” alisema Masha.

Kwa upande wake, Sunga, alisema ameamua kujiunga na CCM kwa sababu ameona inapambana na rushwa na ufisadi kwa vitendo.

“CCM kina dhamira ya dhati ya kuirudisha Tanzania katika misingi yake, inapambana na dhuluma, wizi na unyonyaji,” alisema Sunga.

Mwigamba alisema ameamua kujiuga na CCM ili kuijenga iendelee kudumu na kuwa imara na Serikali yake ifanye vizuri zaidi.

“Tumechagua kutokuwa vuguvugu, tumeamua kuwa moto na wako watu ambao watadhani sisi ni wasaliti, lakini kadiri watakavyopiga kelele tutazidi kuwa wa moto zaidi,” alisema Mwigamba. 

KAULI YA JPM

Baada ya kupokewa kwa wanachama hao, Rais Magufuli alisema ni mfano mzuri wa Watanzania wanaojitambua, lakini akawatahadharisha wasije wakabadilika tena.

“Wako watu wengi wanataka kuingia CCM, leo niliombwa karibu na watu 10 na wengine wamesafiri, lakini kuna wanachama wengine karibu 200 walikuwa viongozi katika mikoa mbalimbali wameamua kurudi CCM.

“Nimeamua wakati mwingine mwafaka tutawakaribisha ili waje wajitambulishe rasmi. Mtembee kifua mbele ninyi ni wana CCM, niwaombe msibadilike tena, msije mkaingia huku kwa majaribio, msimame imara kukitetea chama… hata pakitokea nafasi ya kugombea ya chama ninyi mkagombee tu,” alisema. 

SOPHIA SIMBA ARUDI KUNDINI

Baada ya tukio hilo, Rais Magufuli, alitangaza kusamehewa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Sophia Simba.

Machi 11, mwaka huu, wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Dodoma, Sophia alifukuzwa uanachama kwa madai ya kukisaliti chama katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hatua hiyo ilisababisha apoteze ubunge wa Viti Maalumu na Uenyekiti wa UWT kwani nafasi hizo zinahitaji mtu ambaye ni mwanachama.

Katika kikao hicho, Rais Magufuli, alisoma barua ya Sophia ya kuomba radhi mbele ya wajumbe ambao waliridhia kwa kauli moja kumsamehe kigogo huyo.

Rais Magufuli alisema kati ya wanachama wote waliofukuzwa, Sophia ndiye pekee aliyeandika barua mbili za kuomba radhi.

“Katika wote tuliowafukuza na kuwapa adhabu, huyu (Sophia) ndiye aliandika barua ya kuomba radhi. Amekuwa akiandika barua za kuomba radhi na tumekuwa tukikaa kimya tunamwangalia wala hatumjibu chochote… lakini inaonekana mwenendo wake amekuwa kweli akiomba radhi.

“Wengine wawili waliandika barua kukubaliana na maamuzi yaliyotolewa, lakini wengine walikaa kimya, sasa niliguswa na huyu ambaye aliomba radhi mara nyingi,” alisema.

Rais Magufuli alisoma barua hiyo kisha akawauliza wajumbe kama wanaridhia Sophia asamehewe.

“Sasa nimeona niwaulize wajumbe, mnasemaje tumrudishie uanachama, tumsamehe (wajumbe walinyoosha mikono na kusema asamehewe)… wanaosema sio waseme (hakuna mjumbe aliyesema).

“Katibu Mkuu utamjulisha na mimi nitaandika hapa kwamba NEC imekusamehe,” alisema Rais Magufuli.

 BARUA YA SOPHIA KWA JPM

Sehemu ya barua ya kuomba msamaha iliyoandikwa na Sophia Machi 14, mwaka huu ilisomeka hivi: Mheshimiwa Mwenyekiti kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, niruhusu nichukue fursa hii kukuomba radhi wewe binafsi, wajumbe wa Kamati Kuu, wajumbe wa NEC na CCM kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naikubali adhabu niliyopewa na ambayo ilitolewa na vikao halali vya chama changu, nimeipokea kwa mikono mikunjufu kwani nimekukosea wewe Mwenyekiti wangu na nimekikosea chama changu.

Naandika barua hii kuonyesha majuto yangu kwako na kwa chama changu, naandika barua hii kuomba mnisamehe kwa sababu maisha yangu yote kuanzia kwa wazazi wangu nimekuwa ndani ya TANU na CCM na kila kilichofanikiwa hapa duniani nimekipata kwa sababu ya CCM nikipendacho na kukithamini sana na bado naahidi na namuomba Mwenyezi Mungu anijalie niendelee kuwa mpenzi na mkereketwa wa CCM mpaka mwisho wa maisha yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba radhi tena kwani mzigo huu ni mzito sana na sijui jinsi ya kuubeba, kwani hii ni adhabu yangu ya kwanza kupewa na chama changu, na ndiyo adhabu kubwa na ya mwisho, naomba mnihurumie na Mwenyezi Mungu anihurumie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza sana kwa azma yako ya kuleta nidhamu ndani ya CCM, naamini sana katika chama kuzaliwa upya na katika mabadiliko makubwa ya uchumi wa viwanda, nidhamu na Serikali kwa ujumla.

Naomba nimalize kwa kuomba radhi tena, nisamehe sana na naiomba huruma yako na ya chama changu.

JPM ATAJA VIONGOZI WATAKAOBAKI CCM

Akizungumza katika kikao hicho, Rais Magufuli, alisema viongozi watakaobaki katika chama hicho ni wale tu wenye imani thabiti na mapenzi mema na si CCM masilahi.

Rais Magufuli alisema viongozi wa namna hiyo ndiyo watakaoweza kusimamia Serikali ipasavyo katika ngazi zote.

“Tunahitaji viongozi wachapakazi, waaminifu, waadilifu, wenye kuchukizwa na rushwa, wanaochukia ubadhirifu wa mali za umma na za chama, wapole, wanyenyekevu, lakini wakali kwenye mambo ya ovyo.

“Tunahitaji viongozi wanaoishi imani na ahadi za chama, wasiohongeka, lakini wanaokubalika kwa wanachama na wananchi, si kwa fedha zao bali kwa mienendo yao mema na maono waliyonayo.

“Ukiwa kiongozi wa namna hii chama chetu kitakuwa imara na madhubuti zaidi na kitasimamia haki za wanachama na wananchi wote, hasa wanyonge.

“Viongozi wa namna hii ndio watakaoweza kusimamia Serikali ipasavyo katika ngazi zote na hawa ndio aina ya viongozi ambao chama chetu kinaendelea kuwapata katika uchaguzi wa mwaka huu,” alisema.

Alisema pia mageuzi yanayoendelea kufanywa na chama hicho yamekuwa mwiba mkali kwa wachache ambao walizoea maisha ya kidesturi yasiyoheshimu misingi ya chama.

UCHAMBUZI WA MAJINA

Rais Magufuli alisema wanachama 3,004 walijitokeza kugombea nafasi za uongozi wa mikoa na jumuiya za chama kitaifa wakati nafasi zinazohitajika ni 261.

Alisema majina hayo yalichambuliwa kwa wiki mbili na kwamba kila jina lilichambuliwa pamoja na taarifa nyingine.

 KIKAO KUFANYIKA IKULU

Kuhusu kikao hicho kufanyika Ikulu, Rais Magufuli alisema: “Hapa Ikulu ni kwenu kwahiyo siwezi kuletwa hapa mimi na wana – CCM halafu niwazuie kuja ambako ni kwenu. Tembeeni kifua mbele mmepaandaa ninyi.”

Awali Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 115 kati ya 119 kutoka mikoa 32 nchini. 

BAVICHA WATOA NENO

Akizungumzia na waandishi wa habari jana kuhusu kuondoka kwa wanachama wao na kujiunga na CCM, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrick ole Sosopi, alisema kuwa huu si muda mwafaka wa kuwajadili na badala yake watawatumia ujumbe baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa madiwani.

Alisema kwa sasa wana kazi kubwa ya kujipanga kuhakikisha wanapata madiwani wengi katika chaguzi zijazo.

“Si muda mwafaka kwetu kuwajadili wanaokihama chama, ila tunaamini ni mradi wa chama tawala kuwaaminisha wananchi kama wamebadilika na wanakubalika na ndiyo maana wanawachukua viongozi wetu…

“Historia ya siasa inaonyesha wazi wapo waliohama chama na mambo yakaendelea, hivyo tuna imani tutafaya vizuri zaidi ya sasa kwani tupo imara,” alisema Sosopi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles